Utozwaji wa kodi kwa watu binafsi umegawanyika katika makundi mawili.
- Wafanyabiashara binafsi wadogo walio chini ya mfumo wa makisio ambao hawana uwezo wa kutunza kumbukumbu za biashara zao
- Wafanyabiashara wanaotakiwa na sheria kutunza kumbukumbu za biashara zao.
Mfumo wa Makisio ya Kodi
Huu ni mfumo wa kodi ambapo watu binafsi wasiokuwa na uwezo wa kutunza na kutengeneza hesabu za biashara hutozwa kodi kulingana na makisio ya mauzo yao kwa mwaka. Mlipakodi aliye katika mfumo huu hatakiwi na sheria ya kodi ya Mapato kuandaa na kutuma hesabu za ukaguzi TRA. Hata hivyo, mlipakodi katika eneo hili atakapokuwa na uwezo wa kuweka vizuri kumbukumbu za biashara yake ana hiari ya kutotumia mfumo huu na kuamua kuandaa hesabu za biashara yake zitakazotumika katika ukaguzi na kukokotoa kiwango cha kulipia kodi kulingana na faida aliyopata.
Masharti Yanayokubalika ili Ukadiriwe Katika Mfumo wa Makisio ya Kodi
- Mlipakodi ni lazima awe mkazi
- Mauzo ya mwaka yasizidi kiwango cha Sh. Milioni 100.
- Mapato ya mlipakodi yawe yanatokana na biashara tu katika mwaka wa mapato mengine kama yatokanayo na ajira au uwekezaji. Endapo mapato yatapatikana kutokana na vyanzo vingine kama vile ajira na/au uwekezaji mlipa kodi atatakiwa kutengeneza mahesabu yatakayoyumika katika ukadiriaji wa mapato yake yote kwa jumla na hatoweza kukadiriwa kwa kutumia mfumo huu.
Viwango vya Kodi chini ya Mfumo wa makisio ya Kodi
Chini ya mfumo huu kodi inayolipwa itatokana na mauzo ya mwaka ya mlipakodi kama yalivyo tathiminiwa na Kamishna wa Kodi ya Mapato. Mauzo na viwango vya kodi vimeelezwa hapa chini:
Viwango vya kodi chini ya mfumo wa Makisio ya kodi
Viwango vya kodi kwa wafanyabiashara wadogo wakazi | ||
Mauzo kwa mwaka | Uzingatiaji wa kifungu cha 35 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi (Utunzaji wa Kumbukumbu) | |
Asiyetunza Kumbukumbu za kuridhisha | Anayetunza Kumbukumbu za kuridhisha | |
Mauzo yasiyozidi Sh. 4,000,000/= | Hakuna | Hakuna |
Mauzo yanayozidi sh. 4,000,000/= na hayazidi Sh. 7,000,000/= | Sh.100,000/= | 3% ya mauzo yanayozidi sh. 4,000,000/= |
Mauzo yanayozidi sh.7,000,000/= na hayazidi sh. 11,000,000/= | Sh.250,000/= | Sh. 90,000 + 3% ya mauzo yanayozidi sh.7,000,000/= |
Mauzo yanayozidi sh. 11,000,000/= na hayazidi sh. 100,000,000/= | 3.5% ya mauzo |
Wafanyabiashara Wanaotakiwa Kutunza Kumbukumbu
Hawa ni walipakodi ambao mapato yao ya mwaka yanazidi Sh. 100,000,000. Walipakodi katika kundi hili wanatakiwa na Sheria kutunza kumbukumbu za biashara zao ambazo zitasaidia kutambua kwa ushaihi kiwango cha kodi ya mapato wanachotakiwa kulipa.
Kiwango cha kodi kwa Wanaotunza Kumbukumbu
Walipakodi katika kundi hili wanalipa kwa kuzingatia faida wanazopata. Viwango vinavyohusika katika kundi hili ni kama ifuatavyo:
- Tanzania Bara
Mapato ya mwaka yanayotozwa kodi | Kiwango cha kodi |
Ikiwa jumla ya mapato haizidi Sh. 3,240,000/= | HAKUNA |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 3,240,000/= lakini haizidi Sh. 6,240,000/= | 9% ya kiwango kinachozidi Sh. 3,240,000/=
|
Ikiwa jumla ya mapato inaizidi Sh. 6,240,000/= lakini haizidi Sh. 9,120,000/= | Sh. 270,000/= jumlisha 20% ya kiwango kinachozidi Sh. 6,240,000/= |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 9,120,000/= lakini haizidi Sh.12,000,000/= | Sh. 846,000/= jumlisha 25% ya kiwango kinachozidi Sh. 9,120,000/= |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 12,000,000/=
| Sh. 1,566,000/= jumlisha 30% ya kiwango kinachozidi Sh. 12,000,000/= |
- Zanzibar
Mapato ya mwaka yanayotozwa kodi | Kiwango cha kodi |
Ikiwa jumla ya mapato haizidi Sh. 2,160,000= | HAKUNA |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 2,160,000/= lakini haizidi Sh. 4,320,000/= | 9% ya kiwango kinachozidi Sh. 2,160,000/= |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 4,320,000 lakini haizidi Sh. 6,480,000/= | Sh. 194,400 pamoja na 20% ya kiwango kinachozidi Sh. 4,320,000 |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh.6,480,000 lakini haizidi Sh. 8,640,000/= | Sh. 626,400= pamoja na 25% ya kiwango kinachozidi Sh. 6,480,000 |
Ikiwa jumla ya mapato inazidi Sh. 8,640,000/=
| Sh. 1,166,400/= pamoja na 30% ya kiwango kinachozidi Sh. 8,640,000/= |
Ujazaji wa Taarifa ya Mapato na Ulipaji wa Kodi
Maelezo ya makadirio ya kodi inayolipwa
Mlipakodi atatakiwa kutoa taarifa ya awali ya mapato ambayo mlipakodi anatarajia kupata katika mwaka wa fedha na anapaswa kujaza na kuwasilisha ritani ya makisio hayo kwa Kamishna ndani ya miezi mitatu kuanzia mwanzo wa mwaka wa mapato (ambayo kwa watu binafsi utakuwa ni mwaka wa kalenda unaoanzia Januari hadi Disemba)
Aidha, mlipakodi huyo anatakiwa kuwasilisha na kulipa kodi ya makisio ya mwaka iliyokadiriwa katika kila robo ya mwaka wake wa mapato. Kodi hiyo inapaswa kulipwa kwa awamu zisizozidi nne ambapo kila moja italipwa kila baada ya miezi mitatu. Tarehe za malipo ni kama ifuatavyo:
· Mnamo au kabla ya tarehe 31 Machi
· Mnamo au kabla ya tarehe 30 Juni
· Mnamo au kabla ya tarehe 30 Septemba
· Mnamo au kabla ya tarehe 31 Desemba
Ni wakati gani Mtu binafsi anapaswa kuwasilisha taarifa ya mapato?
Uwasilishaji wa Taarifa (Ritani) ya Mwisho ya Mapato
Mlipakodi anaepaswa kutunza anatakiwa kuwasilisha taarifa ya mwisho ya mapato ndani ya miezi sita tangu tarehe ya kufunga hesabu za mwaka wa mapato. Taarifa hii itaambatishwa na hesabu za mizania za mwenendo wa biashara husika. Ikumbukwe kuwa taarifa hii sio lazima kwa mlipakodi alie chini ya mfumo wa makisio, labda kama ameamua kutunza kumbukumbu za biashara yake.
Mtu binafsi anapaswa kujaza taarifa ya mwisho ya mapato kwenda kwa Kamishna katika kipindi kisichozidi miezi sita baada ya kila mwisho wa mwaka wa mapato.
Kamishna anaweza kuongeza muda wa kujaza taarifa ya mapato kufuatia maombi ya mwombaji kwa maandishi na kwa kuzingatia kanuni na taratibu ambazo Kamishna ataona zinafaa.
Chini ya mfumo wa makisio mtu binafsi halazimiki kujaza fomu yoyote ya taarifa ya mapato badala yake anaweza akalipa kwa awamu kama kiwango kilichokadiriwa kinazidi SHT 50,000 kwa mwaka.
Ni vitu gani muhimu vya kuzingatia wakati wa kujaza taarifa yako ya mapato?
Taarifa ya mapato inakutaka kubainisha mapato yako yatakayotozwa kodi: Hii inahusisha:unapaswa kupitia kurasa za taarifa za fedha za biashara au uwekezaji zilizotumwa pamoja na taarifa ya mapato ili kuhakikisha kwamba kurasa zote zinazotakiwa kwa ajili ya aina mbalimbali za biashara au mapato na faida za uwekezaji zimepokelewa. Kama kuna kurasa zozote zinakosekana au unahitaji kurasa za ziada unatakiwa kuwasiliana na ofisi ya TRA iliyo karibu au kupitia Kituo cha mawasiliano
i. jumla ya mapato yako.
ii. marejesho yoyote ya mapato kutoka katika vyanzo vya kudumu vya mapato ya ndani.
iii. kama hukuwa mkazi wakati wa mwaka wa mapato na kwamba kodi ililipwa kwa zuio na awamu ambapo kulikuwa na mkopo wa kodi kwenye mwaka wa mapato.
Taarifa zilizojazwa zinaweza kuchunguzwa ili kuhakikisha kuwa ni sahihi na adhabu itatolewa kwa atakayetoa taarifa za uongo au kutokuweka mapato. Ikiwa utahitaji msaada wakati wa kujaza taarifa zako, wasiliana na ofisi ya TRA iliyo karibu au kupitia Kituo cha mawasiliano
Ikiwa utahitaji kuongeza muda baada ya muda uliowekwa kujaza taarifa za mapato, utatakiwa kutuma maombi ili kupata idhini ya Kamishna kabla ya muda uliowekwa kisheria kupita.
Baada ya kukamilisha ujazaji wa taarifa yako ya mapato, hakikisha kwamba umejaza taarifa zote zinazohitajika. Ukishakamilisha kujaza, weka saini na tarehe katika tamko lako kisha tuma fomu iliyokamilika TRA. Tuma fomu ikiwa na tarehe ya uthibitisho kwenda TRA. Tuma fomu ikiwa na uthibitisho wa ukokotozi, kurasa za ziada na hesabu zilizokaguliwa (taarifa za fedha). Litakuwa jambo jema kutunza nakala ya fomu iliyojazwa kwa ajili ya kumbukumbu zako.
Ni kumbukumbu zipi zinapaswa kutunzwa na mlipakodi?
Sheria ya kodi inamtaka kila mtu mwenye wajibu wa kulipa kodi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutunza nyaraka zote muhimu ili kuwa na uamuzi sahihi wa kodi inayopaswa kulipwa.
Nyaraka hizi zinapaswa kutunzwa kwa walau miaka mitano kuanzia mwishoni mwa mwaka wa mapato au miaka ya mapato inayohusika isipokuwa ikiwa Kamishna ameelekeza vinginevyo kwa kutoa notisi ya maandishi.
Ikiwa waraka wowote haujaandikwa kwa lugha rasmi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamishna anaweza kumwagiza mhusika kwa maandishi kuleta tafsiri ya lugha rasmi itakayoidhinishwa na kamishna katika notisi, kwa gharama za mhusika.
Je, ni nini maudhui ya fomu ya Ritani?
Fomu ya ritani ina kurasa saba na kuna kurasa zingine za ziada za kukokotoa aina zifuatazo za mapato na faida:
· Faida kutoka kwa utambuzi wa hisa na dhamana katika shirika,
· Manufaa kutoka kwa utambuzi wa mali bila kujumuisha hisa, dhamana au hisa za biashara,
· Mapato yaliyorejeshwa ya uanzishwaji wa kudumu wa ndani wa mtu binafsi,
· Mapato kutoka kwa biashara ya bima ya jumla,
· Mapato kutoka kwa biashara ya bima ya maisha
· Mapato kutokana na shughuli za uchimbaji madini
Kuwasilisha Ritani
· Kukamilisha takwimu katika ritani
Usijumuishe senti - punguza takwimu za mapato, na ujumuishe mikopo ya kodi na makato ya kodi kwa shilingi iliyo karibu zaidi.
· Kuwasilisha Ritani
Usichelewe kuwasilisha ritani, hata kama huna taarifa zote unazohitaji. Pale ambapo baadhi ya maelezo hayapo kadiria kiasi na unaonyesha ni taarifa gani inakadiriwa wakati wa kuwasilisha ambayo inahitaji uthibitisho.
Habari & Matukio
Ufanisi wa Bandari umeongeza mapato ya Serikali
Mwenyekiti wa Bodi aonyesha njia TRA kuvuka malengo