Emblem TRA Logo

Huduma bora kwa mteja ni nguzo muhimu kufikia lengo la ulipaji kodi kwa hiyari.

31 March, 2024

Featured Image

Huduma bora kwa mteja ni nguzo muhimu kufikia lengo la ulipaji kodi kwa hiyari.

Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Bw. Hudson Kamoga amesema kwamba utoaji wa Huduma Bora kwa mteja ni nguzo muhimu sana katika kufikia lengo la Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) la kuwezesha ulipaji kodi kwa hiyari.

Bw. Kamoga ameongeza kuwa wateja wanapopata huduma bora huridhika na kuona fahari kulipakodi kwa hiyari na hatimaye hupunguza au kuondoa kabisa vitendo vya ukwepaji kodi na mienendo ya rushwa.

Kaimu Mkurugenzi Bw. Kamoga ameyasema hayo alipokuwa akifungua rasmi mafunzo ya kujenga utamaduni wa utoaji huduma bora kwa wateja kwa watumishi wa TRA kutoka katika mikoa ya kodi na idara mbalimbali ambao wamechaguliwa kuwa Vinara wa utoaji huduma bora (service champions). Mafunzo hayo yanajumuisha jumla Vinara wa Utoaji Huduma 45 yanayofanyika mjini Morogoro.

“Sote tunafahamu kwamba wateja wetu wanategemea sana ubora wa huduma zetu katika kutimiza majukumu yao ya kisheria ya ulipaji kodi. Hivyo basi, ni jukumu letu kuhakikisha kwamba tunawapatia huduma bora, ili walipe kodi kwa hiyari na hapo tutakuwa tumetimiza jukumu letu la kukusanya kodi kwa uaminifu, weledi, uadilifu na uwajibikaji", alisema Bw. Kamoga.

Aidha, amewahimiza washiriki wote kuyachukua mafunzo hayo kwa umakini na kujituma katika kutoa huduma bora, huku wakizingatia mwongozo wa utoaji huduma kwa tija, (TRA service model) kujifunza kwa bidii, kuweka malengo ya kuendelea kuboresha huduma kila siku. “Tunaweza kufanikiwa kama timu, kwa kushirikiana na kusaidiana kwa pamoja kujenga taswira yetu wenyewe kama watumishi lakini pia kuweka taswira ya Mamlaka yenye chapa (brand) inayoheshimika na kusemewa vizuri na wadau wetu wote wakiwemo watumishi ambao ni wateja wa ndani”, alisisitiza Bw. Kamoga. 

 Kamu Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, watumishi wa TRA hawanabudi kuwatambua wateja wao na tabia zao ikiwemo namna nzuri ya kutunza mahusiano na wateja hao na kuwasikiliza vizuri na kuwahudumia. “Hiki mnachokipata hapa kina maana sana na nyie mtaenda kuisemea vizuri Mamlaka na bahati mbaya sana taarifa nzuri huwa hazisemwi sana kuliko mbaya na bahati mbaya sana taarifa nzuri huwa hazivutii sana kuliko mbaya, hivyo ikitokea kati yetu mmoja akiharibu tujue Mamlaka nzima itasemwa vibaya, tuwe makini katika kuisemea vizuri Mamlaka yetu”, alisema Kamoga.

Kwa upande wao watumishi waliopokea mafunzo hayo wakiwemo Bw. Jeremiah Sarungi kutoka kituo cha Forodha Holili kilichopo mkoani Kilimanjaro na Bi. Johary Urassa kutoka Mkoa wa Kikodi Kariakoo wameipongeza hatua ya TRA kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wake kwani itawasaidia kwa kiwango kikubwa kwenda kuwahudumia walipakodi vizuri na itasaidia kuondoa malalamiko kwa walipakodi na jamii kwa ujumla. 

Hili ni kundi la tatu la kupatiwa ujuzi huu wa utoaji huduma bora katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Sita wa Malaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hii inawafanya watumishi hao kuwa wabobezi wa huduma (Service Champions) kwa kuwa na ujuzi wa kutoa huduma kwa wateja kila mahali ambapo TRA inatoa Huduma.

Vinara wa utoaji huduma ni mmojawapo wa mkakati wa utekelezaji wa mradi wa Chapa (branding) ya TRA uliopo katika mpango mkakati wa sita wa TRA (CP6). Mafunzo yawafanya Vinara hao kuwa na uelewa wa kutoa Huduma bora kwa wateja kila mahali ambapo TRA ina ofisi ambapo kundi linajumuisha watumishi wanaokutana na wateja moja kwa moja na mara nyingi kwa muda mrefu. Hivyo kunauhitaji mkubwa sana kwa kundi hili kuwa na maarifa sahihi ya kuweza kutambua mahitaji na matarajiajo ya mteja kwa haraka ili kukidhi matarajio yao.