Mwenyekiti wa Bodi aonyesha njia TRA kuvuka malengo
19 January, 2023
Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Uledi Mussa amewataka vingozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha zaidi uhusiano wao na wadau wa taasisi mbalimbali za Serekali na wafanyabiashara ili kujenga urafiki na kuongeza ulipaji kodi kwa hiyari.
Mwenyekiti wa Bodi Bw. Mussa ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha Kutathmini utendaji kazi wa TRA kwa nusu ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2022/2023 katika ukumbi wa AICC, Arusha kilichofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 13 Januari, 2023.
Katika kikao hicho Bw. Mussa alitumia fursa hiyo kuwakumbusha na kuwataka viongozi na watumishi wote kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa na pia kufuata sheria za ukusanyaji wa kodi ipasavyo bila ya kumuonea mtu yeyote ili kujenga urafiki na walipakodi na kurahisisha ulipaji kodi kwa hiari.
“Viongozi na watumishi wote kumbukeni kuendelea kusimamia sheria za usimamizi wa kodi ipasavyo na kamwe msimuonee mtu yeyote”, amesema Bw. Mussa.
Sambamba na hilo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Bw. Mussa amewahamasisha watumishi wa TRA kuendelea kufanya kazi kwa bidi, weledi na kwa moyo wa kizalendo kwa kutambua kuwa Bodi inatambua jitihada zao za kuiwezesha serikali kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wote.
“Ninawatia moyo na hamasa kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na moyo wa kizalendo kwani Bodi inatambua mchango wenu wa kuiwezesha serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi”, amesisitiza.
Kwa upande wake Naibu kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Mcha Hassan Mcha amesema tangu kuanza kwa mwaka wa Fedha 2022/2023 TRA imekua ikifanya vizuri kwa kufikia makusanyo ya asilimia 99 katika nusu ya kwanza ya mwaka, lakini licha ya mafanikio hayo amebainisha mambo kadhaa kupitia kila idara ambayo bado hayajafanyiwa kazi ipasavyo na hivyo ameagiza hatua za haraka kuchukuiwa ili kufanya vizuri zaidi katika siku za mbele ili kuweza kufikia na kuvuka malengo ya makusanyo kila mwaka.
Kikao hicho cha siku 5 ambacho kufanyika kila baada ya miezi sita ya utekelezaji wa mpango kazi wa mamlaka, kiliongozwa na Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha na kilifunguliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TRA na mjumbe mwingine Bi. Mariam Nchimbi, viongozi wa juu wa TRA na watumishi wengine kwa lengo la kutathmini utendaji kazi katika nusu ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2022/23 na pia kuweka mipango mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi kwa nusu ya pili ya mwaka