Mashine za Risiti za Kielektroniki ni Nini?
Mashine za Risiti za Kielektroniki ni mashine zilizotengenezwa kwa ajili ya kutumika katika biashara kwa ajili ya kudhibiti usimamizi kwa ufanisi katika maeneo ya uchambuzi wa mauzo na mfumo wa udhibiti wa mali na ambao unafuata masharti yaliyoelezwa na sheria.
Aina za Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD)
- Mashine ya Rejista ya Kodi ya Kielektroniki (ETR)
Mashine hii hutumiwa na wafanyabiashara wa rejareja na wale wanaouza bidhaa kwa kutembeza kwa wateja.
- Printa ya Risiti ya Kielektroniki (EFP)
Mashine hii inatumiwa na vituo vya mauzo ya rejareja vilivyounganishwa kikompyuta. Imeunganishwa kwenye mtandao wa kompyuta na kuhifadhi miamala yote ya mauzo au taarifa zilizowekwa kwenye kumbukumbu zake.
- Chombo cha Kutia Saini za Kielektroniki (ESD)
Kifaa kilichotengenezwa kuthibitisha kwa kusaini waraka wowote wa fedha ulioandaliwa na kompyuta kama vile ankara ya kodi. Kifaa hiki hutumia program maalum ya kompyuta kuzalisha namba maalum (Saini) ambazo huambatishwa na kuchapwa kwenye kila ankara inayotolewa na mfumo wa mtumiaji.
- Mashine ya Kieletroniki ya Printa ya Pampu.
Mashine hii imetengenezwa kwa ajili ya kutumika katika vituo vya mafuta na uchapa kila risiti wakati wa miamala ya mauzo.
ANGALIZO:
Unawajibika kutoa risiti au ankara kwa kila mauzo na kutoa taarifa za mabadiliko/hitilafu zozote za mashine kwa Kamishna ndani ya saa 24. Msambazaji wa mashine atasakinisha, kupanga na kushughulikia hitilafu za mashine ndani ya saa 48
Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) AWAMU YA PILI
Utekelezaji wa awamu ya pili ya Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) ulianza tangu mwaka 2013 kwa lengo la kuongeza idadi ya wafanyabiashara ambao watatumia mfumo wa Mashine za Risiti za Kielektroniki kutoa risiti au ankara za kodi katika kila muamala unaofanyika. Awamu ya pili inajumuisha wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa na VAT unasimamiwa chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato, kupitia Kanuni za Kodi ya Mapato (Mashine za Risiti za Kielektroniki), 2012.
Utekelezaji wa awamu ya pili ya Mashine za Risiti za Kielektroniki utajumuisha makundi yafuatayo;
- Wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa katika kodi ya ongezeko la thamani wenye mauzo-ghafi ya Shilingi milioni 11 na zaidi kwa mwaka;
- Wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo maarufu ya Mkoa, waliobainishwa kwa kuzingatia kodi wanayolipa;
- Wafanyabiashara wanaoshughulikia sekta za biashara zilizochaguliwa kama vile Vipuli, Vifaa vya Ujenzi, Maduka Madogo, Vituo vya Petroli, Maduka ya Simu za Kiganjani, Maduka madogo ya jumla, Baa na Migahawa, Maduka ya Dawa, Maduka ya Vifaa vya Kielektroniki, nk.
Mfumo huu utaendelea na Mamlaka itakuwa inasajili taratibu wafanyabiashara kulingana na ustawi, uzoefu na uwezo wa biashara za wafanyabiashara hao.
Makosa katika umiliki na matumizi ya Mashine za Kieletroniki(EFD)
Makosa kwa kushindwa kutumia mashine za kieletroniki
Mtu yeyote
- Atakayeshindwa kumilki na kutumia mashine ya kieletroniki punde biashara itakapokuwa imeanza au kipindi ambacho kimewekwa na Kamishna kitakapokuwa kimeisha .
- Kushindwa kutoa risiti au Ankara ya kieltroniki punde atakapokuwa amepokea malipoya mauzo ya bidhaa au huduma
- Atakayetoa risiti ya kieletroniki au Ankara ya kieletroniki ambazo si za ukweli au isiyo sahihi kwa namna yoyote ile
- Kutumia mashine za kieletroniki kwa njia ambayo inapotosha mfumo au Kamishna
- Kusababisha au kupelekea mashine ya kieletroniki kutofanya kazi kikamilifu au kwa njia ambayo haitatoa nyaraka ya ukweli au sahihi
Atakuwa ametenda kosa na atawajibika punde atakapopatikana na kosa kwa kulipa faini isiyopungua pointi za sarafu 200 na isiyopungua pointi za sarafu 300 au kifungo kisichozidi miaka mitatu au vyote pamoja.
Makosa haya hayatamhusu mtu ambaye kwa mujibu wa sheria amesamehewa kumilkiau kutumia mashine za kieletroniki.
Pale ambapo kiasi chochote cha kodi kitakuwa kimekwepwa kutokana na kosa lolote;mtu aliyehusika atakapokuwa amebainika kwa nyongeza atalipa faini mara mbili ya kiasi ambacho kimekwepwa au kifungo kisichopungua miaka mitatu.
Mtu ambaye atashindwa kudai risiti ya kieletroniki au kushindwa kutoa taarifa ya kutoa risiti ya kieletroniki au Ankara ya kieletroniki punde atakuwa amefanya malipo ya bidhaa au huduma atakuwa amefanya kosa na ikithibitika atalipa faini isiyopungua pointi za sarafu 2 au isiyopungua pointi za sarafu 100.
Mashine za Risiti za Kielektroniki zina umuhimu gani?
- Zina tunza kumbukumbu za Fedha ambazo haziwezi kufutwa kwa mkono, kemikali au sumaku ya kielektroniki;
- Zinajiendesha zenyewe na kutoa ripoti ya mauzo “Z” kila baada ya saa 24;
- Zinatuma taarifa za kodi moja kwa moja kwenye mfumo wa TRA;
- Zina mfumo wa tarehe usioweza kubadilishwa
- Zinatoa risiti/ankara za kodi za kipekee;
- Zinaweza kutumika zenyewe bila kuunganishwa kwenye mtandao;
- Zina kifaa cha kuhifadhi umeme angalau kwa saa 48, na zinaweza kutumia betri kutoka nje katika maeneo yasiyokuwa na umeme;
- Zinahifadhi data na kumbukumbu zilizowekwa kwenye kumbukumbu za kudumu za fedha moja kwa moja
- Zina uwezo wa kumbukumbu za kodi ambao unahifadhi data kwa takribani miaka 5 au miamala ya siku 1800
- Huepusha migogoro wakati wa ukaguzi na makadirio ya kodi.
- Hurahisisha pingamizi na ukataji wa rufaa za kodi
Wasambazaji wa Mashine za Risiti za Kielektroniki
Habari & Matukio
Ufanisi wa Bandari umeongeza mapato ya Serikali
Mwenyekiti wa Bodi aonyesha njia TRA kuvuka malengo