Utangulizi
Kodi ya zuio ni kiasi cha kodi kinachozuiwa na mtu anapomlipa mtu mwingine kutokana na bidhaa zilizosambazwa au huduma iliyotolewa na mlipwaji. Mtu anayepokea au anayestahili kupokea malipo ambayo kwayo kodi ya mapato inatakiwa kuzuiwa ni mkatwaji wa kodi ilhali mtu anayepaswa kuzuia kodi ya mapato kutoka katika malipo yaliyofanyika kwa mkatwaji anajulikana kama Wakala wa kodi ya zuio.
Malipo yanayostahili kukatwa kodi ya zuio
Kodi ya zuio inatozwa katika malipo husika ikiwa ni pamoja na malipo yanayopaswa kujumuishwa katika kukokotoa mapato ya mwajiriwa yanayostahili kukatwa kutoka kwa mwajiriwa katika ajira, malipo ya mapato ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na magawio, riba, malipo ya maliasili, pango au mrabaha, malipo ya huduma na malipo ya mikataba na malipo ya bidhaa zilizosambazwa serikalini na kwenye taasisi zake.
Taarifa na Muda wa Kulipa Kodi Iliyozuiwa
Kila wakala wa kodi ya zuio atalipa kwa Kamishna kodi ya zuio aliyozuia ndani ya siku 7 baada ya kila mwisho wa mwezi wa kalenda.
Hati ya Kodi ya Zuio
Hati ya kodi ya zuio inapatikana kwenye mtandao kupitia kwenye mfumo wa malipo na Mzuiaji au Mzuiwa anaweza kuipata mara malipo yanapokuwa yamefanyika.
Aina za Kodi za Zuio
Sheria imegawanya kodi ya zuio katika aina kuu mbili, ambazo ni: -
· Kodi za Zuio za mwisho
· Kodi za Zuio zisizo za Mwisho
Kodi za Zuio za Mwisho ni kodi ambazo mzuiwa hawezi kudai punguzo lolote la kodi wakati wa kukokotoa kodi ya mapato inayolipwa kwa mwaka wa mapato.
Kodi za Zuio zisizo za Mwisho: ni kodi ambazo mzuiwa anastahili punguzo la kodi kiasi sawa na kodi inayochukuliwa kuwa imelipwa kwa mwaka wa mapato ambamo kiasi hicho kimekokotolewa.
VIWANGO VYA KODI YA ZUIO | ||
Chanzo cha kodi | Mkazi | Asiye mkazi |
Gawio kwa makampuni yanayomiliki hisa kwa 25% au zaidi | 5% | Hakuna |
Gawio kutoka kwenye makampuni yaliyoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam | 5% | 5% |
Gawio kutoka kwenye makampuni mengine | 10% | 10% |
Malipo mengine ya kodi ya zuio | 15% | 15% |
Riba | 10% | 10% |
Mirabaha | 15% | 15% |
Huduma za kiutawala na kiufundi (Uchimbaji Madini, Mafuta na Gesi) | 5% | 15% |
Watoa huduma za usafirishaji (Ndege/Meli) wasio wakazi/wakodisha ndege wasio na makazi ya kudumu | Hakuna | 5% |
Mapato kutokana na ukodishaji wa nyumba/majengo | 10% | 15% |
Malipo ya bima | 0% | 5% |
Malipo yatokanayo na maliasili | 15% | 15% |
Ada za huduma | 5% | 15% |
Faida ya kuuza hisa, ardhi na majengo | 10% | 20% |
Malipo ya Wakurugenzi (wakurugenzi wasio na ajira za kudumu) | 15% | 15% |
Asilimia ya faida inayotolewa kwa wakala kutoka kwa watoa huduma za utumaji fedha kwa njia ya simu za mkononi. | 10% | Hakuna |
Mauzo yanayohusisha mauzo ya mazao ya Kilimo, mifugo na uvuvi yanapouzwa kwenye Kampuni na Mashirika yote yanayojihusisha na usindikaji na ununuzi wa mazao | 2% Mauzo ghafi | Hakuna |
Malipo kwa bidhaa zilizosambazwa na mtu yeyote kwa serikali na taasisi zake. | 2% kabla ya kukatwa Kodi | Haihusiki |
Kodi ya Pango (Kwa matumizi ya kibiashara) | 10% | 20% |
Malipo mengine ya zuio | 15% | 15% |
Malipo yaliyofanywa kuhusiana na ununuzi wa madini ya thamani, vito na vito vingine vya thamani vilivyotolewa na mwenye leseni ya msingi ya uchimbaji madini au mchimbaji migodi | 2% | N/A |
Malipo yaliyofanywa kwa mkazi kuhusiana na upunguzaji wa hewa ya ukaa iliyothibitishwa | 10% | N/A |
Ndege | 10% | 15% |
Fomu
ITX234.01.E Hati ya Kodi ya Zuio kwenye ada za huduma
Hati/stakabadhi ya malipo kwa ajili ya kodi ya zuio kwa ada za huduma
ITX 230.01.E Taarifa ya kodi ya zuio
Taarifa ya kodi ya zuio na malipo ya kodi iliyozuiwa
ITX 302.01.E Hati/ stakabadhi ya malipo; Kodi ya Zuio kutoka katika riba ya benki.
Hati/ stakabadhi ya malipo kwa ajili ya kodi ya zuio iliyokatwa kutoka kwenye riba ya benki.
Habari & Matukio
Ufanisi wa Bandari umeongeza mapato ya Serikali
Mwenyekiti wa Bodi aonyesha njia TRA kuvuka malengo