Ufanisi wa Bandari umeongeza mapato ya Serikali
10 December, 2024
UFANISI WA BANDARI UMEONGEZA MAPATO YA SERIKALI
KAMISHNA MWENDA.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Mwenda amesema Uwekezaji uliofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam na Kampuni za DP World na ADANI umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Mapato ndani ya kipindi cha miezi Mitano.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilipokwenda Bandarini kujionea shughuli zinazoendelea Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda amesema kuongezeka kwa ufanisi katika uondoshaji wa shehena Bandarini kumeongeza mapato ya serikali.
Kamishna Mwenda amesema pia kwamba, tangu kupitishwa kwa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kumekuwa na ongezeko kubwa la makusanyo ya Kodi kwa kila mwezi na kufikia asilimia 105 hali ambayo imevunja rekodi.
Kamishna Mkuu aliongeza kuwa, uwekezaji na uwepo wa DP World na ADANI Bandarini unahusika na usimamizi wa Bandari lakini mapato yote yanakusanywa na TRA na ndiyo wanatoa kibali cha kutoka kwa mizigo Bandarini baada ya utaratibu kukamilika.
"Uwepo wa DP World na ADANI Bandarini umepunguza siku za Meli kukaa nangani zikisubiri kupakua mizigo kutoka siku 37-25 na sasa ni siku 4-5 ambapo Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha hakuna Meli inayosubiri kushusha mzigo" Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda.
Kwa upande wa Msimamizi wa Kampuni ya DP World Bw. Elitunu Malamia amesema wanahudumia Gati no. 1 mpaka 7 kwa mizigo ya kawaida maarufu kama Kichere pamoja na magari yanayokwenda katika nchi jirani za Afrika Mashariki huku mengine yakitumika nchini.
Malamia amesema kasi waliyokuwa nayo katika kuhudumia mizigo ni kubwa ambayo imeongezeka kwa asilimia 20 na wanao uwezo wa kuhudumia mpaka makontena 800 ndani ya saa 24 huku akiomba kuongezwa kwa idadi ya Gati za kushushia mizigo.
Naye Msimamizi wa Kampuni ya ADANI Bwa. Donald Talawa amesema wao wahudumia mizigo ya makasha na wanatumia Gati namba 8 mpaka 11 huku nao wakiwa wameongeza ufanisi kwa asilimia kubwa na kasi ya kuondosha mizigo na kwa Mwezi December pekee wanatarajia kuhudumia makasha 77,000.
Kwa upande wa Wabunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Oran Njeza amesema Kamati haikutarajia kukutana na kazi kubwa kwa viwango walivyovikuta na kuwapongeza wawekezaji wa DP World na ADANI kwa kuongeza ufanisi na TRA kwa kuongeza makusanyo ya mapato.