Emblem TRA Logo
Kodi katika Huduma za Kieletroniki

Kuanzishwa kwa Sheria ya Kodi ya Mapato na Kodi ya Ongezeko la Thamani katika huduma za kielektroniki

Kwa upande wa Kodi ya Mapato; Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 ilifanyia mabadiliko Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 kwa kuongeza kifungu cha 69(m) ili kutambua malipo yanayofanywa na watumiaji wa huduma wasiofanya biashara kwa ajili ya huduma zitolewazo na wafanyabiashara wasio wakaazi kuwa ni malipo ambayo chanzo chake ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, kifungu cha 90A cha Sheria ya Kodi ya Mapato kinawapa watoa huduma za kielektroniki wasio wakaazi wajibu wa kulipa kodi ya mapato kwa kiwango cha asilimia mbili (2%) kutokana na malipo wanayopokea kwa huduma wanazotoa kutipita masoko ya kidijitali kutoka kwa watumiaji walio katika Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wasiofanyabiashara.

Hata hivyo, Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023, ilifanyia mabadiliko kifungu cha 90A cha Kodi ya Mapato, Sura 332 kwa kujumuisha huduma zote za kielektroniki na si zile tu zinazotolewa kupitia masoko ya kidijitali ili kuongeza wigo wa kodi.

Kwa upande wa Kodi ya Ongezeko la Thamani; Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022 iliifanyia mabadiliko Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148 kwa kuongeza kifungu cha 64(5) ili kuwezesha wafanyabiashara wasio wakaazi kuweza kujisajili pasipokuwa na takwa la kuwa na mwakilishi wa kodi.

Vilevile, Kanuni za Kodi ya Mapato (Usajili wa watoa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) za Mwaka 2022 na Kanuni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (Usajili wa wasambazaji wa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) za Mwaka 2022, zilitungwa ili kutoa mwongozo wa namna ambavyo mabadiliko ya Sheria yanapaswa kutekelezwa.

Utekelezaji wa Sheria 

A: Usajili

  1. Kanuni ya 4 ya Kanuni za Kodi ya Mapato (Usajili wa watoa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) ya Mwaka 2022 na Kanuni ya 4 ya Kanuni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (Usajili wa wasambazaji wa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) ya Mwaka 2022 zinamtaka mfanyabiashara wa huduma za kielektroniki asiye mkaazi anayestahili kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria, kuwasilisha ombi la kujisajili kwa Kaminshna Mkuu kupitia njia ya mtandao uliyorahishwa.
  2. Hakuna kigezo cha kuwa na kiwango cha mauzo ili kustahili kujisajili.

B: Uwasilishaji wa ritani na Malipo

  1. Kanuni ya 6 ya Kanuni za Kodi ya Mapato (Usajili wa watoa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) ya Mwaka 2022 na Kanuni ya 6 ya Kanuni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (Usajili wa wasambazaji wa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) ya Mwaka 2022 zinamtaka mfanyabiashara wa huduma za kielektroniki asiye mkaazi kuwasilisha ritani na kufanya malipo ya kodi kwa njia ya mtandao. 
  2. Kifungu cha 90A (2) cha Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 na Kanuni ya 6 ya Kanuni za Kodi ya Ongezeko la Thamani (Usajili wa wasambazaji wa huduma za kielektroniki wasio wakaazi) (Marekebisho) ya Mwaka 2023 zinaainisha tarehe 20 ya mwezi unaofuata kuwa tarehe ya kuwasilisha ritani na kufanya malipo ya kodi ya mwezi husika.
  3. Kiwango cha Kodi ya Mapato (Kodi ya Huduma za Kieletroniki) ni asilimia mbili (2%) ya Mapato ghafi.
  4. Kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani ni 18%.
  5. Madai ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya manunuzi hayaruhusiwi.
  6. Watoa huduma/wasambazaji wa huduma za kielektroniki hawana wajibu wa kutumia mashine za kielektroniki (EFD) wanapotoa risiti. 
  7. Kodi italipwa kupitia akaunti ya benki itayoidhinishwa na Kamishna Mkuu.
  8. Kodi italipwa kwa Shilingi ya Tanzania au fedha nyingine yenye thamani inayolingana na Shilingi ya Tanzania kwa mujibu wa viwango vya kubadili fedha vitakavyotelewa na Benki Kuu ya Tanzania katika siku ambayo malipo yatafanyika.

Kuanzishwa kwa Kodi ya zuio Katika Maudhui ya Kidijitali na Mali za Kidijitali

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 iliifanyia mabadiliko Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 kwa kuongeza kifungu cha 83B kinachowapa wafanyabiashara wakaazi na wasio wakaazi wanaowalipa watengeneza maudhi ya kidijitali wakaazi wajibu wa kuzuia kodi kwa kiwango cha asilimia tano (5%) ya malipo hayo.

Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024 iliifanyia mabadiliko Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 kwa kuongeza kifungu cha 83C kinachowapa wamiliki wa majukwaa ya kielektroniki ya kubadili mali za kidijitali au wanaowezesha ubadilishaji au uhamishaji wa mali za kidijitali na kuwalipa wakaazi, wajibu wa kuzuia kodi kwa kiwango cha asilimia tatu (3%) ya malipo hayo.