Emblem TRA Logo
Pingamizi na rufaa za kodi

Sheria inayosimamia Pingamizi na Rufaa za Kodi

Pingamizi  na rufaa  zinasimamiwa na Sheria ya usimamizi wa kodi na. 438 rejeo la 2019 na sheria ya Rufaa ya Kodi Na. 408 rejeo la mwaka 2019 na marekebisho yake mara kwa mara.

Utangulizi kuhusu Pingamizi na Rufaa

Sheria za Kodi Tanzania inamruhusu mtu yeyote anayehisi kuwa amenyimwa haki kuomba mabadiliko rasmi ya maamuzi rasmi kuhusiana na makadirio ya kodi yaliyofanywa na Kamishna Mkuu. Mlipakodi anayehisi kuwa Kamishna Mkuu ametumia vibaya sheria, amefikia kupata matokeo ambayo si sahihi, alitumia vibaya mamlaka yake, alikuwa na upendeleo, alizingatia ushahidi ambao hakupaswa kuuzingatia au ameshindwa kuzingatia ushahidi ambao angepaswa kuuzingatia katika kufanya makadirio ya kodi, anaweza kupinga makadirio hayo

Makadirio ya Kodi na Migogoro

Huu ni ukadiriaji wa kodi kama unavyoongozwa au kuhalalishwa na kila sheria ya kodi inayohusika.

Makadirio yenye Mgogoro

Haya ni makadirio ambayo yamefanywa na Kamishna Mkuu na mlipakodi hakubaliani na matokeo ya makadirio hayo.

Kodi Isiyokuwa katika Mgogoro

Hii ni kodi ambayo haina mgogoro kwa pande zote mbili.

Namna ya Kushughulikia Pingamizi na Rufaa

Taratibu za Kuweka Pingamizi na Kukata Rufaa

Mtu yeyote ambaye hakubaliani na maamuzi ya kodi aliyofanyiwa anapewa nafasi kuwasilisha pingamizi la makadirio hayo. Pingamizi linapaswa kuwa katika maandishi na kutumwa kwa Kamishna Mkuu. Pia yawe na ujumbe ambao ni mahususi, ukielezea msingi wa pingamizi kwa makadirio yaliyofanywa.

Rufaa itakatiwa wapi na kuwasilishwa kwa nani?

Kamishna wa Forodha, Idara ya Walipa Kodi Wakubwa, na Kodi za Ndani. Hata hivyo ushughulikiaji wa rufaa unafanywa na mameneja wa maeneo husika.

Ushughulikiaji wa Kodi zenye Mgogoro

Itabidi kuwasilisha pingamizi kwa Kamishna Mkuu ndani ya siku 30 tangu siku ya kupokea makadirio kusubiri uamuzi wa mwisho. Wakati wa kipindi cha pingamizi kutegemea uamuzi wa mwisho wa pingamizi kwenye makadirio yaliyofanywa na Kamishna Mkuu, mlipakodi huyo anawajibika kisheria kulipa kiasi cha kodi ambacho hakipo kwenye mgogoro au theluthi moja ya kodi iliyokadiriwa, kiasi chochote kilicho kikubwa. Hata hivyo, ikiwa Kamishna Mkuu ataridhika kwamba kuna sababu za msingi kuruhusu kupunguza au kuondoa kodi itakayolipwa wakati wa pingamizi hilo anaweza kuagiza kuwa kiasi kidogo kilipwe au asamehe kiasi kinachotakiwa cha malipo ya kodi.

Kodi ambayo haina mgogoro italipwa wakati wa kufungua shauri la pingamizi na kama tarehe ya kulipa imefika mapema kuliko kipindi cha siku 30 kodi ambayo haina mgogoro italipwa katika tarehe hiyo husika. Kiasi cha kodi kama kitakavyoamuliwa mwishoni baada ya kusuluhisha pingamizi hilo, kama kitakuwa kidogo kuliko kiasi kilicholipwa kwa Kamishna Mkuu kitarejeshwa kwa anayepinga. Kuhusu suala la kodi au ushuru uliokadiriwa kwenye kodi, kiasi chote kilichokadiriwa kitachukuliwa kuwa hakipo katika mgogoro.

Kuchelewa Kuwasilisha Pingamizi la Makadirio ya Kodi

Mlipakodi anaweza kushindwa kuweka pingamizi kwa wakati dhidi ya makadirio ya kodi. Hata hivyo, sheria bado inampa nafasi mtu huyu kuweka pingamizi baada ya kipindi husika kupita. Kamishna anaweza kukubali au kukataa pingamizi kutegemea kuridhishwa au kutoridhishwa na sababu za kuchelewa huko.

Kamishna anaweza kukubali kupokea pingamizi lililochelewa kuwekwa kwa kuzingatia sababu zifuatazo:

Sababu za Msingi za Kupokelewa kwa Pingamizi

Kama Kamishna Mkuu ameridhika kuwa sababu za kuchelewa ni kutokuwepo kwa mlipakodi katika Jamhuri ya Muungano;

 Kama Kamishna Mkuu ameridhika kuwa sababu za kuchelewa ni ugonjwa;

Sababu nyingine za msingi baada ya kuridhika kwa Kamishna Mkuu. 

Uthibitisho wa Kodi Iliyokadiriwa na Kamishna

Kamishna Mkuu, baada ya kupokea pingamizi, kwa mujibu wa kifungu cha 12, ataamua pingamizi kama lilivyowasilishwa au anaweza kuitisha ushahidi wowote kadri atakavyoona inafaa kwa ajili ya kutolea uamuzi, na kwa msingi huo anaweza–

   (a) Kurekebisha makadirio kwa mujibu wa pingamizi;

   (b) Kurekebisha makadirio kwa mujibu wa ushahidi wowote uliopokelewa; au anaweza kukataa kurekebisha makadirio ya kodi.

Pale ambapo Kamishna Mkuu amekubali kurekebisha makadirio kwa misingi ya pingamizi atatoa waraka wa makadirio ya mwisho kwa mtoa pingamizi. Au-

   (a) Atapendekeza marekebisho kwa kuzingatia pingamizi na vielelezo vingine vilivyoletwa; au

   (b) Atapendekeza kukataa kurekebisha makadirio na atamtumia waraka mtoa pingamizi akieleza sababu za kukataa.

Baada ya kupokea waraka/taarifa mtoa pingamizi, ndani ya siku 30 atawasilisha waraka wa maandishi kwa Kamishna Mkuu kueleza kukubaliana au kupinga mapendekezo ya makadirio yaliyorekebishwa au yaliyokataliwa.

Kamishna Mkuu anaweza, baada ya kupokea waraka wa mtoa pingamizi kufanya yafuatayo:

(a) Kuamua kuhusu pingamizi kwa kuzingatia mapendekezo ya makadirio yaliyorekebishwa au yaliyokataliwa na wasilisho lolote lilifanywa mtoa pingamizi; au

(b) Kuamua kuhusu pingamizi kiasi fulani kwa kuzingatia wasilisho la mtoa pingamizi; au

(c) kuamua kuhusu pingamizi kwa mujibu wa marekebisho yaliyopendekezwa au yaliyokataliwa.

Pale ambapo mtoa pingamizi hajajibu mapendekezo ya Kamishna Mkuu ya kurekebisha makadirio au pendekezo la kukataa kurekebisha makadirio yaliyotolewa kulingana na kifungu kidogo cha (3), Kamishna Mkuu ataendelea kufanya makadirio ya mwisho ya kodi na kumpatia mtoa pingamizi taarifa kuhusu maamuzi yaliyotolewa.

Ngazi za Rufaa

Kimsingi, kuna ngazi tatu ambapo mlipakodi anaweza kukata rufaa ikiwa hajaridhishwa na maamuzi ya Kamishna Mkuu.

Rufaa kwenda katika Bodi:

Sheria inaeleza kuwa, mtu yeyote ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa mwisho wa makadirio yaliyofanywa na Kamishana Mkuu anaweza kukata rufaa kwenye bodi. Bodi itapokea rufaa kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:

1   Notisi ya rufaa itolewe ndani ya siku 30 tangu Kamishna Mkuu atoe uamuzi wake wa mwisho wa makadirio ya kodi kwa mkata rufaa; na

2)     Rufaa iwasilishwe kwenye Bodi ya rufaa ndani ya siku 45 tangu tarehe ambayo taarifa ya uamuzi wa mwisho ya makadirio ya kodi ulipotolewa kwa mkata rufaa;

3)    Taarifa hiyo itoe maelezo yote kuhusu makadirio ya kodi na mawasiliano zaidi yaliyofanyika kati ya Kamishna Mkuu na mlipakodi.

Kukata Rufaa katika Baraza la Kodi

Baada ya uamuzi wa Bodi kufanyika, mlipakodi anaweza kuona kuwa bado hajaridhishwa na uamuzi huo. Mlipakodi ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa bodi anaweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwenye Baraza la kodi. Rufaa kwenye Baraza la kodi itazingatia yafuatayo:

1)  Rufaa ikatwe ndani ya siku 30 tangu tarehe ya kufanyika uamuzi wa Bodi na mkata rufaa atapeleka taarifa kwa upande pinzani ndani ya siku 15 tangu siku ambayo taarifa ya rufaa iliwasilishwa mahakamani.

2)   Bodi au mahakama inaweza kurefusha ukomo wa muda uliowekwa kwa mujibu wa sheria kama imeridhishwa kuwa kushindwa kwa upande huo kutoa taarifa ya rufaa, kupinga rufaa au kutoa taarifa kwa upande pinzani kulitokana za sababu zifuatazo:

Rufaa katika Mahakama ya Rufaa

Mtu yeyote ambaye hajaridhishwa na uamuzi wa mahakama anaweza kuamua kukata rufaa katika mahakama ya rufaa.

Pale ambapo Mtoa pingamizi anaamua kukata rufaa katika Bodi au Mahakama kodi yoyote inayotakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria itaendelea kulipwa  wakati Kamishna Mkuu akisubiri uamuzi wa mwisho  wa rufaa.