Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi
Utangulizi
Tozo ya uendelezaji ufundi stadi (SDL) ni ushuru unaotozwa chini ya Kifungu cha 14 cha Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Sura ya 82, na hukusanywa na TRA.
Utozwaji
SDL hutozwa kwa kuzingatia jumla ya malipo yote anayolipa mwajiri kwa waajiriwa wake katika kipindi husika (mwezi). Ni muhimu kufahamu kuwa SDL ni wajibu wa mwajiri kulipa.
Jumla ya malipo ni mkusanyiko wa fedha zinazotokana na mishahara, ujira, malipo ya likizo, ada, kamisheni, bonasi, gratuity, posho za kujikimu, usafiri, burudani au posho nyingine yoyote anayopokea mfanyakazi kutokana na ajira au huduma aliyotoa.
Iwapo mwajiri atalipa malipo kwa mfanyakazi kwa vipindi visivyo vya kila mwezi (chini au zaidi ya mwezi), malipo hayo yatachukuliwa kana kwamba mfanyakazi analipwa kila mwezi, na kiwango cha malipo kinachotozwa kwa mwezi kitahesabiwa kana kwamba malipo yalikuwa ya kila mwezi.
Nani anawajibika kulipa SDL?
Mwajiri yeyote mwenye wafanyakazi kumi (10) au zaidi anatakiwa kulipa SDL kutokana na jumla ya malipo.
Viwango vinavyotumika:
Kiwango cha SDL ni asilimia 3.5 ya jumla ya malipo yote yaliyolipwa kwa wafanyakazi katika mwezi husika. Hii inahusisha wafanyakazi wa kudumu, wa muda, wa ziada, vibarua, n.k.
Wajibu wa Mwajiri
- Kuhesabu kiasi cha ushuru na kulipa kwenye akaunti ya Kamishna katika ofisi ya kodi ya eneo alilosajiliwa.
- Kufanya malipo ya SDL kwa kutumia fomu ITX 300.01.E - Employment Taxes Payment Credit Slip.
- Kuandaa na kuwasilisha taarifa ya kila mwezi kupitia IDRAS kabla au ifikapo tarehe 7 ya mwezi unaofuata.
- Kuandaa na kuwasilisha cheti cha nusu mwaka kinachoendana na taarifa za kila mwezi zilizowasilishwa.
Wanaosamehewa SDL
SDL haitozwi kwa:
- Idara za Serikali au taasisi za umma zinazofadhiliwa kikamilifu na Serikali;
- Misheni za Kidiplomasia;
- Umoja wa Mataifa na taasisi zake;
- Taasisi za kimataifa au za kigeni zinazojihusisha na misaada au msaada wa kiufundi;
- Taasisi za kidini ambazo wafanyakazi wake wanajihusisha tu na:kuendesha ibada; kutoa mafundisho ya dini; kusimamia shughuli za kidini; kutoa huduma za afya ya jamii;
- Mashirika ya misaada (charitable organizations);
- Taasisi za elimu zilizosajiliwa, zikiwemo: shule za awali, msingi na sekondari; vyuo vya ufundi na mafunzo; vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu;
- Mamlaka za Serikali za Mitaa;
- Wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo walio chini ya mpango wa Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA);
- Waajiri wa mashambani ambao wafanyakazi wao wanajihusisha moja kwa moja na shughuli za kilimo (isipokuwa wale wanaosimamia au kushughulika na usindikaji wa mazao).
Maana ya Shirika la Misaada
Ni taasisi ya ndani yenye maslahi ya umma inayokidhi masharti yafuatayo:
(a) Ilianzishwa na inaendeshwa kwa madhumuni ya:
kupunguza umaskini au mateso ya jamii;
kuendeleza elimu; au
kutoa huduma za afya ya jamii, elimu, maji, au ujenzi na matengenezo ya barabara;
(b) Imetolewa hati ya utambuzi na Kamishna chini ya Kifungu cha 11 cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya 438, kuthibitisha kuwa ni shirika la misaada au la kidini.
Kumbuka:
Misamaha kwa Zanzibar inahusu vipengele (a–d) na (g) pekee vilivyotajwa hapo juu.
Marekebisho ya Sheria:
Kifungu cha 19 cha Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (Sura ya 82) kimefanyiwa marekebisho kumpa Waziri mwenye dhamana ya Fedha mamlaka, baada ya kushauriana na Waziri husika, ya kutoa msamaha wa ushuru huu pale inapokuwa kwa manufaa ya umma.
Habari & Matukio