Emblem TRA Logo

MHE. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atoa tuzo kwa walipakodi bora kwa mwaka 2023/2024

24 January, 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan amewataka Walipakodi nchini kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuacha vitendo vya ukwepaji Kodi ambavyo vinaondoa usawa wa ushindani sokoni.

 

Akizungumza wakati wa utolewaji wa Tuzo za Mlipakodi January 23, Jijini Dar es Salaam Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema utolewaji wa tuzo hizo unachochea ulipaji wa Kodi kwa hiari na kuwataka wenye tabia za kukwepa kodi kuacha mara moja kwani wanadhoofisha Uchumi wa Nchi na kuwavunja moyo Walipakodi waaminifu kwa kuweka ushindani usiokuwa sawa sokoni.

 

Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo wameandaa tuzo hizo kuendelea kupambana na watu wanaokwepa Kodi kwa kuwasaka wanaoghushi risiti za EFD na VFD pamoja na wanaotumia Stempu bandia kwenye vinywaji.

 

"Dhuruma siyo kitu kizuri hivyo wanaokwepa Kodi watambue kuwa wanafanya dhuruma Hali kadhalika watumishi wa TRA wanaofanya makadirio yasiyokuwa sahihi nao wanafanya dhuruma, tuache" Dk. Samia.

 

Dk. Samia amesema mwelekeo wa Serikali ni kuongeza idadi ya Walipakodi na siyo kuwatumia wachache waliopo na Hali hii itafanikishwa na kurasimisha sekta isiyo rasmi ili iwe rasmi na kulipa Kodi kikamilifu.

 

Rais Samia amesema Ilani ya Uchaguzi ya CCM inaitaka Nchi ipunguze utegemezi na utegemezi huo utapungua kwa kusimamia kwa usahihi ukusanyaji wa Kodi jambo ambalo litaifanya Tanzania ijiamini.

 

Rais Samia amesema Bajeti ya Serikali ni Sh. Trilion 49.34 na miongoni mwa fedha hizo Sh. Trilion 30.4 sawa na asilimia 61.6 inatokana na makusanyo ya Kodi kutoka kwa TRA hiyo ndiyo inaonyesha tunavyouendea kujitegemea hivyo ongezeni juhudi katika kukusanya Kodi.

 

Rais Samia amesema Mwaka ujao 2025/2026 hakutakuwa na Tuzo za Mlipakodi za TRA bali kutakuwa na Tuzo za Rais ili kuonyesha umuhimu wa kulipa Kodi.

 

"Kwenye masuala ya Kodi hakuna mzaha,  mtu asijifanye kwamba ana maelekezo kutoka juu asilipe Kodi, napenda kuwaambia hakuna mtu yoyote niliyemruhusu asilipe Kodi na Mimi ndiyo ngazi ya juu ya mwisho, kama nitamruhusu mtu yoyote nitatoa maagizo kwa barua" Rais Samia 

 

Kuhusu masuala ya kesi za kikodi ameitaka Bodi ya rufani kuharakisha usikilizaji wa kesi hizo ili Kila mmoja apate haki yake.

 

Rais Samia ametoa rai kwa watumishi wa TRA kufanya kazi kwa uaminifu, kudumisha nidhamu kwa kuwa na mienendo mizuri kazini ili kuwajengea Imani Walipakodi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi tuzo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna baada ya benki hiyo kuibuka mshindi wa jumla katika kipengele cha Mlipakodi wa hiari wa kampuni na mwenye kiasi kikubwa cha mchango wa kodi kwa mwaka 2023/24 katika sekta mbalimbali za kiuchumi wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa walipakodi bora kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambayo imefanyika tarehe 23 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba aliyeambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Uledi Abbas Mussa pamoja na Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa Walipakodi bora kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambayo imefanyika tarehe 23 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam.