Kodi ya Ongezeko la Thamani ni nini?
Kodi ya Ongezeko la Thamani ni kodi ya mlaji inayotozwa katika bidhaa zinazostahili kutozwa kodi, ikiwa ni pamoja na huduma, mali zisizohamishika na shughuli yoyote ya kiuchumi wakati wowote thamani inapoongezeka katika kila hatua ya uzalishaji na katika hatua ya mwisho ya mauzo. Kodi ya Ongezeko la Thamani inatozwa kwa bidhaa zote zinazozalishwa ndani na huduma na kwenye maduhuli. Kodi ya Ongezeko la Thamani anatozwa mtu aliyesajiliwa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani tu.
Mawanda ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ni yapi?
Kodi ya Ongezeko la Thamani itatozwa katika usambazaji wowote wa bidhaa, huduma na bidhaa zisizohamishika za shughuli yoyote ya kiuchumi Tanzania Bara ambapo ni usambazaji unaotozwa kodi unaofanywa na mlipa kodi katika shughuli ya kiuchumi anayofanya. Uingizaji wa bidhaa zinazokatwa kodi kutoka sehemu yoyote nje ya Tanzania Bara zitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani na Sheria za Kawaida za Forodha na taratibu zitatumika. Bidhaa zote zitakazotumika nje ya Tanzania Bara hazitatozwa Kodi ya Ongezeko la Thamani baada ya kupata uthibitisho. Kodi ya Ongezeko la Thamani itatozwa kwa bidhaa na huduma zinazotozwa kodi. Viwango sanifu vya Kodi ya Ongezeko la Thamani ni 18% na 0% kwa bidhaa zinazosafirishwa nje ya nchi.
Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani ni lazima kwa kila mtu aliyefikia kiwango cha juu cha usajili cha milioni 200 kwa kipindi cha miezi 12 na mtu aliyefikia mauzo ghafi ya kiwango cha nusu (100 milioni) au zaidi ya usajili kwa kipindi cha miezi sita.Sharti hili linahusu aina zote za usajili isipokuwa kwa watoa huduma za kitaalamu,mashirika ya umma,taasisi zinazohusika na shughuli za kiuchumi na mfanyabiashara kusudio baada ya kukidhi vigezo vya uthibitisho kama mikataba,zabuni,mpango wa ujenzi,mpango wa biashara na ufadhili wa benki. Sharti hili linahusu aina zote za usajili isipokuwa kwa watoa huduma za kitaalamu.
Mtu anayetakiwa kusajiliwa analazimika kufanya maombi kwa kamishna mkuu ndani ya siku thelathini (30) lakini kwa mfanyabiashara kusudio anaweza kufanya maombi hayo wakati wowote.Kamishna mkuu atamsajili mtu yoyote na VAT pale atakapojiridhisha kuwa mtu huyo anatakiwa kusajiliwa kwa ajili ya kulinda mapato ya serikali na hajafanya hivyo, atamsajili na kumtaharifu ndani ya siku 14 toka siku ya usajili bila kujali kiwango chake cha mauzo ghafi.
Mchakato wa Usajili
Maombi ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani yanafanyika mtandaoni kupitia Dirisha la Mlipakodi (Taxpayer Portal) lililopo kwenye tovuti ya TRA baada ya muombaji kuigia kwenye mfumo.
Cheti cha Usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
Kufuatia usajili, mlipakodi atapewa cheti cha usajili kikitaja jina na mahali ambapo ilipo biashara ya mlipakodi, tarehe ambayo usajili umefanyika na namba ya utambulisho wa mlipakodi na namba yake ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani.
Mtu huyo ataonesha namba ya utambulisho wa mlipakodi na namba yake ya usajili wa Kodi ya Ongezeko la Thamani katika taarifa yoyote, hati ya rufaa au nyaraka nyingine zinazotumika kwa shughuli rasmi Zinazohusu Kodi ya Ongezeko la Thamani na kutundika cheti chake cha usajili katika sehemu ambayo inaonekana kwa urahisi katika eneo lake la biashara.
Taarifa ya VAT na Malipo ya Kodi
Taarifa ya VAT ni fomu inayotumika kuwasilisha malipo ya kodi kwenda Mamlaka ya Mapato. Kwa sasa wafanyabiashara waliosajiliwa katika VAT wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao za mapato katika ofisi za Mamlaka ya Mapato kwa njia ya mtandao tu kupitia lango la mlipakodi.
Uwasilishaji wa Ritani ya VAT kwa bidhaa na huduma zitolewazo hapa nchini, itawasilishwa siku ya 20 ya mwezi unaofuata mwezi wa biashara, Endapo siku ya tarehe 20 itaangukia Jumamosi, Jumapili au Sikukuu ritani ya VAT itawasilishwa siku ya kwanza ya kazi inayofuata Jumamosi, Jumapili au Sikukuu.
Viwango vya Kodi
Viwango vipi hutumika kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani?
Kodi ya Ongezeko la Thamani hutozwa katika bidhaa na huduma stahiki kwa viwango vifuatavyo :-
Na. |
Viwango vya VAT Aina ya bidhaa na au huduma zinazohusika |
Kiwango cha VAT |
1 | Bidhaa na huduma zinazotozwa kodi - Tanzania bara | 18% |
2 | Uagizaji na uingizaji wa bidhaa na huduma toka nje kuingia Tanzania bara. | 18% |
3 | Uuzaji wa bidhaa nje ya nchi. | 0% |
4 | Kutomhusisha mpitishaji bidhaa kulipa VAT kwa gharama ya huduma ya usafirishaji wa bidhaa/mizigo iendayo nje ya nchi kupitia Tanzania Bara, huduma zinajumuisha:- | |
| I. Huduma zinazohusiana moja kwa moja na bidhaa inayopitishwa kwenda nje ya nchi
| 0% |
| I. Bidhaa zilizohifadhiwa kwenye bandari, uwanja wa ndege au maeneo ya forodha kwa kipindi kisichozidi siku 30 zikisubiri kusafirishwa |
0% |
Kodi ya Ongezeko la Thamani inatozwaje?
Kila mtu aliyesajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani katika mlolongo kati ya msambazaji wa kwanza na mnunuzi au mtumiaji wa mwisho, anatozwa kodi kwenye bidhaa alizouziwa (kodi kwenye manunuzi) na atatoza kodi kwa bidhaa atakazo uza (kodi kwenye mauzo). Analipa Mamlaka ya Mapato ziada ya kodi kwenye mauzo juu ya kodi kwenye manunuzi, au anarudishiwa ziada ya kodi kwenye manunuzi juu ya kodi kwenye mauzo. Katika mfumo huu biashara huwa haziathiriki isipokuwa mfanyabiashara anatakiwa kukusanya kodi hiyo kutoka kwa mnunuzi na kuiwasilisha TRA.
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ni fedha anazorejeshewa mfanyabiashara. Mlipakodi atastahili kurejeshewa Kodi ya Ongezeko la Thamani iwapo katika kipindi husika cha mahesabu, taarifa zake za kodi zinaonyesha kodi kwenye manunuzi ni kubwa kuliko kodi kwenye mauzo. Marejesho huandaliwa na kulipwa kwa mlipakodi kupitia Mfumo wa Malipo kati ya Benki na Benki (TISS) au kupitia akaunti yake ya benki.
Mlipakodi anaweza kuomba kurejeshewa kodi pale anapokuwa amelipa zaidi ya kiwango halisi cha kodi kinachotakiwa kulipwa kwa kipindi hicho; maombi yanaweza kutumwa kupitia fomu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ITX260.02E ikiambatishwa na:
1. Hati ya kuthibitisha uhalali wa madai;
Hati ya madai husika itatolewa chini ya kanuni ndogo na mkaguzi wa hesabu aliyesajiliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu na aliyesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama mshauri wa masuala ya kodi;
2 Ukokotoaji wa Kiasi cha marejesho;
a. Orodha ya marejesho ya malipo ya kodi ya ongezeko la thamani ya mwombaji; na
b. Na taarifa nyingine zozote kadri Kamishna Mkuu atakavyozihitaji.
Baada ya kupokea madai ya marejesho Kamishna Mkuu anafanya uamuzi kuhusu maombi kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa bila kufanyiwa ukaguzi au uchunguzi na ndani ya siku 90 za kupokea maombi hayo atafanya uamuzi kuhusu maombi hayo na kumwarifu mwombaji kuhusu kiasi cha kurejeshewa na muda wa kusubiri marejesho kufanywa.
MAREJESHO YA KODI YA ONGEZEKO LA THAMANI KWA WANADIPLOMASIA NA MASHIRIKA YA KIMATAIFA
Maombi ya kurejeshewa kodi kwa wanadiplomasia na mashirika ya kimataifa yatatumwa kwa Kamishna Mkuu
Je, Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Yanaweza Kufidia Kodi ambayo Haijalipwa?
Ndiyo. Marejesho yoyote ya kodi yanaweza kufidia kodi nyingine, adhabu, na riba ambazo mlipa kodi anayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, lakini Kamishna Mkuu atamjulisha mlipakodi kwa maandishi.
Je, riba inalipwa kwa marejesho yaliyocheleweshwa?
Ndiyo. Marejesho yanapaswa kufanyika ndani ya siku 30 baada ya tarehe ya kuwasilisha taarifa ya kodi kwa kipindi cha mwisho cha hesabu katika nusu mwaka au kupokea taarifa za malimbikizo ya mwisho ya kodi husika kwa kipindi chochote husika cha hesabu kinachoangukia ndani ya nusu mwaka huo, chochote kilichokuja baadaye isipokuwa kama Kamishna anaamini kuwa kuna hatari ya mapato. Kwa wafanyabiashara wanaolipa mara kwa mara marejesho yatafanyika ndani ya siku 30 baada ya tarehe ya kutoa taarifa ya kodi kwa kipindi husika cha hesabu, au tarehe ya kupokea taarifa ya kodi, yoyote iliyo ya baadaye.
Iwapo marejesho hayo hayatafanyika katika kipindi hiki, riba inalipwa kwa mlipakodi katika benki ya biashara, kiwango cha mkopo kikiamuliwa na Benki Kuu.
Masharti Gani ya kuzingatia ili Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani yaweze Kufanyika?
Marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani hayawezi kufanyika isipokuwa kama mwombaji amewasilisha miongoni mwa mambo mengine nyaraka na/au viambatisho vifuatavyo:
1. Hati ya uhalali inayotolewa na mkaguzi wa hesabu ambaye amesajiliwa na Bodi ya Wahasibu na wakaguzi wa hesabu nchini na ambaye amesajiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama mshauri wa ya kodi.
2. Orodha ya taarifa za masuala ya maombi ya marejesho ya VAT inapaswa kujazwa na kukamilishwa kwa usahihi na mwombaji.
3. Kwa suala la wafanyabiashara wanaolipa mara kwa mara, nyaraka zifuatazo ni muhimu kuwasilishwa:
- Hati ya tamko la uingizaji wa bidhaa (TANSAD)
- Hati ya taarifa ya mizigo iliyopo kwenye meli
- Hati ya kusafirishia mizigo kwa Ndege
- Hati ya taarifa ya mizigo inayosafirishwa kwa njia ya barabara
- Hati ya ardhi
- Risiti/ankara za kielektroniki
4. Ripoti fupi ya mkaguzi wa hesabu kuonesha namna kiasi kinachodaiwa kimepatikana ikiwemo muhtasari wa manunuzi na mauzo.
Angalizo: Marejesho hayatakatwa/hayatatolewabaada ya miezi sita tangu tarehe ya Ankara ya kodi/risiti za EFD.
Nafuu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
Unafuu wa VAT kwa Mwekezaji chini ya EPZ, SEZ na Kampuni za Madini, Mafuta na Gesi
Mwekezaji aliyepewa leseni chini ya usindikaji wa mauzo ya nje au Sheria za eneo maalum la kiuchumi ana haki ya kupata unafuu maalum wa VAT. Makampuni ya uchimbaji madini, mafuta na gesi yana haki ya kupata unafuu wa VAT mradi tu Kampuni ina makubaliano ya lazima na Serikali ambayo yanatoa unafuu wa VAT.
Ili kufurahia Wawekezaji na makampuni yenye haki ya uchimbaji madini wanalazimika kujaza fomu: ITX263.02. E. Fomu inaweza kupatikana kutoka ofisi yoyote ya TRA iliyo karibu nawe au unaweza kuipakua kupitia tovuti ya TRA.
Kuahirishwa kwa bidhaa za mtaji Uahirishaji unamaanisha kuahirishwa kwa malipo ya ushuru wa ongezeko la thamani katika bidhaa za mtaji. Kuahirishwa kwa bidhaa za mtaji zilizoagizwa kutoka nje sio moja kwa moja kama ilivyo kwa maombi ya mwombaji; maombi yatachunguzwa na kuidhinishwa na Kamishna.
VAT iliyojumuishwa kwenye kila kitengo cha bidhaa iliyoagizwa lazima iwe na kipengele cha VAT kinachozidi 20,000,000. Kuahirishwa ni kutokana ndani ya miaka kumi. Bidhaa zinazoingizwa nchini ambazo VAT yake ni chini ya 20,000,000/- zitachukuliwa kama kawaida na zitafuata kanuni za kawaida za ukokotoaji wa kodi kwa sheria na taratibu za Forodha.
Wakati mfanyabiashara anaagiza bidhaa kuu, ushuru uliotofautiana utachukuliwa kama kodi ya pato na kodi ya pembejeo ya mwagizaji wakati wa uagizaji na itahesabiwa kwenye marejesho ya kodi sawa. Pale ambapo muda wa kuahirishwa unapita ushuru uliotofautiana hautalipwa. Uahirishaji uliotolewa lazima uwe wa kutengeneza bidhaa zinazotozwa ushuru na sio msamaha wa usambazaji
Malipo na Uwasilishaji wa Uthibitisho wa Malipo
Mamlaka ya Mapato imechukua hatua kadhaa kuboresha utendaji wake kwa kutumia mfumo unaorahisisha na kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa walipakodi.
Ili kuwa na mifumo ya malipo iliyo salama na yenye ufanisi, taasisi hizi mbili, yaani Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania zilikubaliana kuweka mfumo wa pamoja ambao umeboresha mchakato wa ukusanyaji mapato na kufanikisha kuwa na Mchakato wa Utendaji wa Moja kwa moja kati ya TISS-CBS katika Benki Kuu ya Tanzania na EPICOR, ITAX na TANCIS katika Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mfumo wa kulipia kodi kwa njia ya mtandao na Benki ni mfumo unaoweza kutambua miamala ya malipo ya kodi inayofanywa na mlipakodi kati ya Benki kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania, na kwa lengo la kuboresha ukusanyaji wa mapato.
Njia tatu za kulipa kodi kwa mtandao:
- Malipo ya mapato kupitia Mfumo wa Malipo baina ya Benki (TISS) kwenda moja kwa moja Benki Kuu ya Tanzania (Ujumbe wa SWIFT)
- Malipo ya kodi kupitia benki yanayoonekana moja kwa moja kwenye mifumo maalum ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, mapato yanayohamishiwa Benki Kuu ya Tanzania kufanyika baadaye
- Malipo kwa njia ya simu za mkononi.
Mfumo huu unafanyaje Kazi?
Mfumo huu wa malipo mtandaoni utawawezesha walipakodi kujisajili kwa kusudio la kulipa kodi kupitia mfumo ulioandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mlipakodi atachagua njia ya malipo ya TISS; baada ya kuwasilisha RG itaandaa hati ya malipo na kutoa namba maalumu ya uhakiki; Namba ya uhakiki, ambayo ina tarakimu kumi na mbili itatumika kufanya ulinganishaji wa hesabu kati ya Mamlaka ya Mapato na Benki za Biashara. Mlipakodi hatimaye atawasilisha hati ya malipo katika Benki ya Biashara; na kuagiza Benki ihamishe fedha kwenda kwenye akaunti ya Kamishna katika Benki Kuu ya Tanzania; Benki ya Biashara itapokea stakabadhi na kuagiza hamisho kwa kuanzisha muamala katika SWIFT Terminal kwa kuonesha namba ya uhakiki wa hati. Njia ya uingizaji mapato itapokea taarifa za muamala kwa njia ujumbe wa SWIFT kutoka TISS na kuthibitisha na kubadili miamala hiyo; mwisho, Njia ya uingizaji mapato itaingiza taarifa mpya katika mfumo husika wa mapato kupitia huduma zake za wavuti.
Njia ya uingizaji mapato inaokoa muda wa walipakodi muda katika mchakato wa malipo; itaboresha hesabu na uchanganuzi wa makusanyo ya mapato ya serikali; inapunguza ushiriki wa binadamu katika miamala ya ulipaji wa kodi; inaboresha ukamilifu wa data na kuongeza kazi ya mchakato wa uandaaji wa nyaraka.
Pia njia ya kukusanyia mapato inaongeza usalama kwa kuwa idadi kubwa ya ujumbe wa malipo unaingia; inapunguza gharama kwa kuwa Mamlaka ya Mapato itadumisha mfumo mmoja kwa benki zote za biashara ambao utakuwa rahisi kuusimamia na kuuhudumia; taratibu za malipo kwa mlipakodi zimerahisishwa na Mamlaka ya mapato Tanzania inapokea uthibitsho wa malipo kila malipo yanapofanyika.
Uwasilishaji wa Taarifa kwa njia ya Mtandao
Uwasilishaji wa taarifa ya kodi kwa njia ya mtandao una maana gani?
Huu ni mfumo wa uwasilishaji wa taarifa za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania kupitia tovuti yake www.tra.go.tz
Taratibu zipi zinapaswa kufuatwa?
Uwasilishaji wa taarifa za Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa njia ya mtandao unapasa kufuata hatua zifuatazo:
Wasilisha Rejesho la VAT
- Ingia kwenye www.tra.go.tz
- Ingia lango la mlipa kodi (taxpayer portal)
- Ingiza number ya mlipakodi (TIN) na nywila
- Chagua kampuni unayotaka kurejesha faili
- Nenda huduma ya kurejesha faili
- Bonyeza mwezi husika wa kurejesha file
- Fuata stepu mfumo utakao kupa
Faida za kuwasilisha taarifa kwa njia ya mtandao
Uwasilishaji wa taarifa kwa njia ya mtandao una faida zifuatazo:
- Walipakodi watakuwa wanawasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania wakiwa majumbani au maofisini mwao
- Kupunguza foleni katika ofisi za TRA
- kuondoa au kupunguza foleni kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania katika tarehe za mwisho za uwasilishaji wa taarifa za kodi
- Uwasilishaji wa taarifa kwa njia ya mtandao unapunguza makosa na unarahisisha mchakato wa nyaraka
Msamaha wa VAT kwa miradi inayofadhiliwa na serikali au wafadhili
Kamishna Mkuu anaweza, baada ya maombi ya mwombaji katika fomu iliyowekwa, kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye;
(a) uingizaji wa malighafi zitakazotumika pekee katika utengenezaji wa vyandarua vya muda mrefu na mtengenezaji wa ndani wenye mkataba wa utendaji kazi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
(b) uagizaji kutoka nje wa taasisi ya serikali au usambazaji kwa chombo cha serikali wa bidhaa au huduma zitakazotumika tu kwa utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na-
(i) Serikali;
(ii) mkopo wa masharti nafuu, mkopo usio na masharti nafuu au ruzuku kupitia makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na serikali nyingine, mfadhili au mkopeshaji wa mkopo wa masharti nafuu au mkopo usio na masharti nafuu; au
(iii) mkataba wa ruzuku ulioidhinishwa ipasavyo na Waziri kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana ya Serikali iliyoingiwa kati ya mamlaka ya serikali za mitaa na mfadhili: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma hiyo;
(c) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya maafa ya asili au maafa/majanga.
(d) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi iliyo na makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa madhumuni ya kuendesha au kutekeleza mradi wa kimkakati: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma;
(e) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa shirika lisilo la kiserikali lenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya mradi unaotekelezwa na asasi isiyo ya kiserikali inayohusika: msamaha kwa bidhaa au huduma.
Kumbuka: Msamaha uliotolewa chini ya sehemu hii utakoma kufanya kazi na ushuru wa ongezeko la thamani utalipwa na kulipwa kana kwamba msamaha haujatolewa ikiwa bidhaa au huduma zilizotajwa zinahamishwa, kuuzwa au kutupwa kwa njia yoyote kwa mwingine. mtu asiye na haki ya kufurahia marupurupu sawa na yaliyotolewa chini ya Sheria hii.
Msamaha kwa Uwekezaji Ulioidhinishwa na NISC
Waziri, baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri na kwa agizo lililochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, atatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa au huduma kwa ajili ya utekelezaji wa uwekezaji maalum wa kimkakati ulioidhinishwa na Kamati ya Kitaifa ya Uendeshaji Uwekezaji chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania.
Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani
Kamishna Mkuu anaweza, baada ya maombi ya mwombaji katika fomu iliyowekwa, kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye-
(a) uingizaji wa malighafi zitakazotumika katika utengenezaji wa vyandarua vya muda mrefu pekee.
(b) kuingiza au kusambaza kwa taasisi ya Serikali ya bidhaa au huduma zitakazotumika tu kwa utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na- (i) Serikali. (ii) mkopo wa masharti nafuu, mkopo usio na masharti nafuu au ruzuku kupitia makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na serikali nyingine, mfadhili au mkopeshaji wa mkopo wa masharti nafuu au mkopo usio wa masharti nafuu. (iii) makubaliano ya ruzuku yaliyoidhinishwa ipasavyo na Waziri kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana ya Serikali iliyoingiwa kati ya mamlaka ya serikali ya mitaa na mfadhili: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma.
(c) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya maafa ya asili au maafa.
(d) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa taasisi iliyo na makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa madhumuni ya kuendesha au kutekeleza mradi wa kimkakati: Isipokuwa kwamba, makubaliano hayo yanatoa msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa au huduma;
(e) uingizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa shirika lisilo la kiserikali lenye makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya mradi unaotekelezwa na asasi isiyo ya kiserikali inayohusika: msamaha kwa bidhaa au huduma. Waziri anaweza, kwa utekelezaji bora wa masharti ya kifungu hiki, kutunga kanuni zinazoainisha namna ya maombi, utoaji na ufuatiliaji wa matumizi ya msamaha uliotolewa.
f) Kuuzwa kwa nyumba yenye thamani isiyozidi shilingi milioni 50 na mtengenezaji wa majengo.
g) Usambazaji wa madini ya thamani, vito na vito vingine vya thamani kwenye viwanda vya kusafishia, vituo vya ununuzi au Majumba ya Madini na Vito yaliyoundwa na Tume ya Madini chini ya Sheria ya Madini.
h) Kuagiza au kusambaza ndege, injini ya ndege, sehemu za ndege na matengenezo ya ndege kwa mwendeshaji wa ndani wa usafiri wa anga.
i) Ugavi wa vifaa vya magari vinavyotumika kubadilisha mfumo wa mafuta ya gari kuwa gesi asilia au mfumo wa umeme kwa watu wanaofanya ubadilishaji wa magari hayo.
j) Uagizaji wa makasha ya kutengenezea maumbo ya dawa zinazotumiwa na mtengenezaji wa ndani wa dawa kwa matumizi ya kipekee katika utengenezaji wa bidhaa za dawa Tanzania Bara.
Bidhaa zinazouzwa kati ya Bara na Zanzibar
Pale ambapo kwa upande wa usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa kodi, kodi ya ongezeko la thamani imelipwa Tanzania Zanzibar kwa kiwango cha chini kuliko kiwango kinachotumika Tanzania Bara chini ya Sheria hii, tofauti ya kodi ya ongezeko la thamani itahesabiwa kuwa haijalipwa. na zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kutoka kwa mtu anayetozwa kodi baada ya kuhamishwa kwa bidhaa kwenda Tanzania Bara kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii.
Iwapo kuhusiana na usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa kodi, usambazaji huo unafanywa moja kwa moja na mtu anayetozwa kodi Tanzania Bara kwa mpokeaji ambaye ni mtu anayetozwa kodi Tanzania Zanzibar, Mamlaka ya Mapato Tanzania itakusanya kodi ya ongezeko la thamani na kuituma kwa Bodi ya Mapato ya Zanzibar.
Pale ambapo kwa upande wa usambazaji wowote wa bidhaa unaotozwa kodi, ushuru umelipwa Tanzania Zanzibar kwa mujibu wa sheria kwa wakati unaotumika Tanzania Zanzibar, kwa kiwango sawa na kiwango kinachotumika Tanzania Bara, kodi hiyo itahesabiwa kuwa zimelipwa kwenye usambazaji unaotozwa kodi kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii na hakuna kodi itakayolipwa baada ya uhamisho wake kwenda Tanzania Bara.
Habari & Matukio
Ufanisi wa Bandari umeongeza mapato ya Serikali
Mwenyekiti wa Bodi aonyesha njia TRA kuvuka malengo