WCO YASISITIZA MAGEUZI YA KIDIJITALI NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KUIMARISHA FORODHA DUNIANI
14 May, 2026
Katibu Mkuu wa Shirika la Forodha Duniani (WCO), Bw. Ian Saunders, amesema kuwa changamoto zinazoikumba sekta ya forodha duniani zinaongezeka kila mwaka kutokana na mabadiliko ya kasi ya biashara ya kimataifa, hivyo kuhitaji ushirikiano wa karibu, matumizi ya teknolojia za kisasa na uimarishaji wa mifumo ya usimamizi wa mipaka.
Bw. Saunders ameyasema hayo Alhamis Mei 14, 2026 wakati akihutubia Mkutano wa 32 wa Baraza la Uongozi la Shirika la Forodha Duniani Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (WCO ESA) unaofanyika Zanzibar- Tanzania, ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama kushirikiana kikamilifu kukabiliana na changamoto za mnyororo wa usambazaji wa bidhaa pamoja na uhalifu wa mipakani.
Amesema mabadiliko ya biashara ya dunia yanayoambatana na ukuaji wa biashara mtandao, matumizi ya akili mnemba (AI) na maendeleo ya teknolojia yanahitaji mageuzi makubwa ya kidijitali ndani ya taasisi za forodha ili kuongeza ufanisi na uwazi katika huduma.
Aidha, ameeleza kuwa ufanisi wa forodha unategemea ushirikiano wa karibu kati ya mamlaka za sheria, wadhibiti wa mipaka na sekta binafsi ili kulinda biashara halali dhidi ya uingizaji wa bidhaa haramu na vitendo vya uhalifu wa kiuchumi.
Bw. Saunders amesisitiza kuwa mustakabali wa forodha duniani unahitaji uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya kidijitali, uboreshaji wa taratibu za kiutendaji na ushirikiano endelevu wa kimataifa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya biashara ya dunia.
Akihitimisha hotuba yake, ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na kuimarisha mshikamano wa kikanda na kimataifa katika kuendeleza sekta ya forodha kwa manufaa ya uchumi wa dunia.
Habari Mpya