Emblem TRA Logo

KITUO CHA KODI WAZO NI SEHEMU YA UTEKELEZAJI WA KUSOGEZA HUDUMA ZA KODI KARIBU NA WANANCHI– CG MWENDA

17 September, 2026

Katika kuendelea kuboresha huduma za kodi kwa wananchi, Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imeendelea kufungua vituo vya kodi maeneo ya pembezoni karibu na wananchi vikiwemo vya Wazo na Mbezi Beach vilivyopo kwenye mkoa wa kodi Tegeta jijini Dar es Salaam.

Ili kuona ufanisi wa vituo hivyo, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amefanya ziara Wazo na Mbezi Beach kwa lengo la kuona huduma zinavyotolewa na kuzungumza na Walipakodi kwa lengo la kusikiliza na kuzitatua changamoto zao.

Akiwa katika ziara hiyo Kamishna Mkuu Mwenda amesema wameamua kusogeza huduma za kodi karibu na wananchi ili kuokoa muda wao wa kufanya biashara na kutoa wito kwao kuzitumia ofisi hizo kutatua changamoto zao za kodi na kupata huduma nyingine za kodi.

"Tumewasogezea karibu huduma za kodi zitumieni kuboresha biashara zenu kupitia Dawati la uwezeshaji biashara ambalo lipo katika kila kituo, na uwepo wa vituo hivi umesaidia kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari" amesema Bw. Mwenda.

Kwa upande wake Kamishna wa Kodi za Ndani Bw. Michael Muhoja amesema TRA itaendelea kuwafuata wananchi walipo maana ni jukumu lake kuwahudumia na kurahisi ulipaji wa kodi kwa wananchi.

Meneja wa mkoa wa Kodi Tegeta Bw. Dickson Qamara amesema ongezeko la vituo vya kodi mkoani humo litaongeza zaidi wigo wa kodi kupitia usajili wa walipakodi wapya waliopo kwenye miji ya pembezoni inayochipukia.