Emblem TRA Logo

UTARATIBU MPYA WA TRA WAHARAKISHA UINGIZAJI MAFUTA YA VYOMBO VYA MOTO SOKONI

30 March, 2026

Utaratibu mpya wa kutoa mafuta kwenye vituo vya kuhifadhia mafuta ya Dizeli na Petroli kwenda sokoni uliowekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), umetajwa kuharakisha utoaji wa mafuta kwenye vituo vya kuhifadhia kwenda sokoni.

Utaratibu huo wa kikodi unawataka wamiliki wa mafuta hayo kuyalipia kodi kabla ya kuyaingiza sokoni ili yanapoingizwa sokoni yanaendelea na taratibu za uuzwaji hali ambayo inarahisisha usambazaji na kuwafikishia wateja huduma ya mafuta kwa wakati.

Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amefanya ziara kwenye baadhi ya vituo vya kuhifadhia mafuta ya vyombo vya moto jijini Dar es Salaam leo tarehe 29.03.2026 kikiwemo kituo cha Camel Oil, Moil Energies na Mount Meru na kujiridhisha namna utaratibu huo mpya unavyofanya kazi.

Akiwa katika ziara hiyo Kamishna Mkuu Mwenda amezungumza na wasimamizi wa vituo hivyo ambao wamemuhakikishia uwepo na mafuta ya kutosha kwenye viyuo hivyo na namna  utaratibu mpya wa TRA unavyorahisisha utoaji mafuta na kuweka udhibiti.

Aidha amesema TRA imejiwekea utaratibu wa kufanya kazi kwa saa 24 ili kuharakisha utolewaji wa huduma kwa walipakodi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti waratibu na wasimamizi wa vituo vya kuhifadhia mafuta akiwemo Omar Yusufu wa Mount Meru amesema utaratibu huo mpya wa TRA umeonyesha mafanikio makubwa kwa kusaidia uingizaji mafuta sokoni kwa urahisi.