Emblem TRA Logo

TRA KUENDELEA KULINDA VIWANDA VYA NDANI ILI KUONGEZA WIGO WA KODI

19 May, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo inaendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuendelea kulinda viwanda vya ndani ili kuongeza wigo wa kodi ikiwemo kupambana na uingizaji wa bidhaa nchini bila kufuata utaratibu.

Ameyasema hayo leo Mei 18, 2026 alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mount Meru Group inayojihusisha na uzalishaji wa mafuta ya kupikia ya Alizeti na Pamba Bw. Atul Mittal kwenye ofisi za TRA jijini Dar es Salaam.

Kamishna Mkuu amesema TRA inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa kodi kutoka kwenye viwanda vya ndani hivyo imekuwa ikifanya kila jitihada ili kuvilinda na kumpongeza Mkurugenzi huyo wa Mount Meru Group kwa kuwekeza katika sekta ya mafuta ya kupikia na kulipa kodi kwa hiari na kutoa wito kwa wafanyabiashara wengine nao kufuata nyayo zake kwa kulipa kodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya Taifa.

Katika mazungumzo hayo mfanyabiashara huyo Bw. Atul Mittal ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kupambana na magendo ya mafuta ya kupikia ambayo yamekuwa yakichangia kudhoofisha viwanda vya ndani, kuinyima Serikali Mapato na kuondoa ushindani wa biashara sokoni.


Bw. Mittal amesema udhibiti wa magendo kwenye mafuta ya kupitia unaviongezea nguvu viwanda vya ndani vya mafuta ya kupikia ambavyo ni takribani 4,000 kwa nchi nzima na kuwahakikishia wananchi usalama wa afya zao huku akiipongeza TRA kwa kuwa na mfumo wa kodi unaotabilika na kumuwesha Mlipakodi kujua alipe kiasi gani kwa mwaka mzima.