Emblem TRA Logo

WAZIRI WA FEDHA AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA OFISI YA TRA KIZIMKAZI

14 August, 2026

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zinazotarajiwa kujengwa Kizimkazi Visiwani Zanzibar lengo likiwa ni kusogeza karibu na Wananchi huduma za Kodi. 
 
Akiweka jiwe hilo la msingi Agosti 13, 2026 Balozi Khamis Mussa Omar amesema kupitia ofisi hiyo itakayowahudumia wananchi wa Kizimkazi na Paje pamoja na ofisi nyingine za TRA zilizopo nchi nzima huduma za kodi zitaboreka zaidi na kuwapunguzia wananchi kadhia ya kufuata huduma mbali na maeneo yao.
 
Balozi Omar amesema maendeleo makubwa yanayoonekana nchini yanatokana na Kodi za wananchi na kuipongeza TRA kwa juhudi inazofanya katika kukusanya kodi za wananchi na kuvuka malengo wanayopangiwa na Serikali ambapo kwa mwezi Julai pekee kwa  mwaka wa fedha 2026/2027 walitakiwa kukusanya Sh. Trilioni 2.971 lakini imekusanya Sh. Trilioni 3.245 sawa na asilimia 109 na ukuaji asilimia 21.
 
Amesema kukusanya kodi ni mzunguko wa ukuaji wa uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja na kuwataka watanzania waone fahari kulipa kodi kwani watakuwa wamechangia katika maendeleo ya Taifa. 
 
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imeweka mkakati wa kuendelea kusogeza karibu zaidi huduma na wananchi kwa kujenga ofisi nyingi na kwa mwaka wa fedha wanatarajia kujenga jumla ya ofisi 49 kwa nchi nzima. 
 
Amesema lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi ni kutaka kuokoa muda wa wananchi kufanya shughuli zao za kiuchumi. 
 
Amesema TRA itaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi wote bila kumpendelea wala kumuonea mtu huku akiweka wazi kuwa wataendelea kupambana na wote wanaokwepa kodi na kutoa rai kwa wananchi kuwafichua.