Emblem TRA Logo

CG MWEMDA AWEKA WAZI HAKI ZA WALIPAKODI

24 April, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa kuzingatia haki za walipakodi, ikiwemo kuhakikisha uwazi, usawa na upatikanaji wa huduma kwa wakati ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Akizungumza leo Aprili 24, 2026 katika Kongamano la Maadili katika Ukusanyaji wa Kodi pamoja na Uzinduzi wa Jukwaa la Maadili kwa wadau wa TRA, lililofanyika katika Ukumbi wa Johari Rotana, Kamishna Mkuu huyo amesema TRA ina Mkataba wa Huduma kwa Mlipakodi unaobainisha aina ya huduma zinazotolewa pamoja na muda wa kuzipata.

Amesema mamlaka hiyo itaendelea kuweka wazi haki za walipakodi, akisisitiza kuwa miongoni mwa haki hizo ni kusikilizwa, kulindwa kwa taarifa zao, kutendewa usawa kwa mujibu wa sheria na kukadiriwa kodi sahihi kulingana na taratibu zilizowekwa.

Aidha, ameeleza kuwa kila tathmini ya kodi lazima iambatane na nyaraka maalumu ili kuhakikisha uwazi na uhalali wa makadirio hayo, huku akibainisha kuwa TRA imeweka utaratibu wa kila Alhamisi kuwa siku maalum ya kuwasikiliza walipakodi nchini ili kutatua changamoto zao.

Kwa upande mwingine, Kamishna Mkuu huyo amewataka walipakodi kutimiza wajibu wao kwa kuzingatia sheria za kodi, ikiwemo kutokwepa kodi, kusajili biashara zao, kutoa taarifa sahihi za mapato pamoja na kushirikiana na watumishi wa TRA katika utekelezaji wa majukumu yao.

Pamoja na hayo amesisitiza umuhimu wa kuepuka vitendo vya rushwa na kuhakikisha utoaji wa risiti kwa kila mauzo yanayofanyika, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi, kuimarisha uaminifu na hatimaye kukuza mapato ya Serikali kwa maendeleo ya taifa.