KAMISHNA MKUU TRA AKUTANA NA WADAU WA SEKTA YA MADINI, KUIMARISHA USHIRIKIANO NA UWEZESHAJI BIASHARA
02 September, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amekutana na uongozi wa kampuni za Geita Gold Mine na Barrick Gold Mine katika kuendelea na juhudi za TRA za kuwafikia na kuwasikiliza walipakodi, hususan wadau wa sekta ya madini, kwa lengo la kujadili changamoto za kikodi, kuimarisha ushirikiano na kuwezesha shughuli za biashara nchini.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Septemba 02, 2026 katika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam, uongozi wa kampuni hizo umeeleza kufurahishwa na utaratibu wa TRA wa kufungua milango na kukutana na walipakodi ili kusikiliza changamoto zao na kujadili namna bora ya kuwezesha biashara. Wamesema hatua hiyo imekuwa na mchango katika kuongeza uelewa wa masuala ya kodi, kujenga mahusiano mazuri kati ya TRA na walipakodi na kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu Mwenda amezipongeza kampuni hizo kwa mchango wao katika uchumi wa nchi kupitia uwekezaji na ulipaji kodi, akieleza kuwa TRA itaendelea kuwafikia walipakodi katika maeneo yao, kusikiliza changamoto zao na kutafuta suluhisho kwa wakati. Amesema Mamlaka itaendelea kuboresha huduma na mifumo ya kodi pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kurahisisha shughuli za biashara na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Aidha, Kamishna Mkuu Mwenda amesema ushirikiano wa karibu kati ya TRA na sekta ya madini ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za uwekezaji zinaendelea kukua sambamba na ulipaji kodi kwa hiari na upanuzi wa wigo wa kodi. Amesema TRA inatambua na kuthamini mchango wa walipakodi wakubwa na kwamba milango ya Mamlaka ipo wazi kwa wadau wote kwa ajili ya kusikilizwa, kuwezeshwa na kushirikiana katika kuongeza mchango wa sekta mbalimbali katika maendeleo ya Taifa.