Habari & Matukio
TRA YAANZA KUCHUKUA HATUA UTARATIBU MPYA UINGIZAJI MAFUTA YA KULA
25 March, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema tayari Mamlaka hiyo imeanza kuchukua hatua kuelekea kuanza kutumika kwa utaratibu mpya wa kuingiza mafuta ya kula Tanzania Bara kutoka Zanzibar.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Machi 24.2026 jijini Dar es Salaam Kamishna Mkuu Mwenda amesema miongoni mwa hatua zilizoanza kuchukuliwa ni kuunda kamati ndogo ya wataalam inayohusisha Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko, maofisa wa Forodha na waagizaji wa mafuta kwaajili ya kuweka utaratibu utakaoanza kutumika kuingiza mafuta hayo hivi karibuni.
Amesema utaratibu huo mpya unalenga kuwezesha biashara ya Mafuta baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuchangamsha biashara katika Bandari za Bagamoyo, Mbweni na Kunduchi ambazo ndiyo hutumika kuingiza mafuta hayo.
"Tutatoa punguzo kwa mafuta yanayoingia Tanzania Bara kutoka Zanzibar ili kuwawezesha wanaoingiza mafuta hayo kupata faida, Serikali kupata kodi na pia kulinda viwanda vya ndani" amesema Bw. Mwenda.
Kamishna Mkuu Mwenda amewaonya wafanyabiashara wa mafuta watakaojihusisha na magendo baada ya kuanza kutumika kwa utaratibu huo kuwa Serikali haitasita kuwachukuli hatua kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu amesema TRA itaendelea kutoa elimu ya kodi kwa wananchi wote na kuwezesha biashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. Ali Suleiman Ameir imeipongeza TRA kwa uwajibikaji na kuahidi kuwa wataendelea kushirikiana nayo katika kuieleza jamii umuhimu wa kulipa kodi.
Habari Mpya