Habari & Matukio
TRA NA URA KUSHIRIKIANA KUPAMBANA NA UKWEPAJI KODI
25 March, 2026
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) zimekubaliana kushirikiana katika kupambana na ujwepaji wa kodi kwa kuzuia magendo yanayofanyika baina ya nchi hizo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Viongozi wa URA nchini Tanzania wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo Bw. Emmanuel Katonge wakati wa kikao kilichofanyika ofisi za TRA jijini Dar es Salaam Machi 25.2026 Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili wanaweza kuzuia magendo.
Amesema TRA imekuwa na uhusiano mzuri wa muda mrefu na URA katika utendaji kazi na kubadilishana taarifa huku akionya wafanyabiashara wa mchele wasiokuwa waaminifu wanaoingiza mchele nchini Uganda na kusema umetoka Tanzania wakati siyo kweli kwamba wakibainika watawajibishwa.
Aidha Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kuwezesha biashara baina ya nchi hizo mbili huku ikiwezesha uwepo wa maofisa wa URA katika Idara ya Forodha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya URA Bw. Emmanuel Katonge amesema wataendelea kushirikiana na TRA katika masuala ya kodi na kuzia uingizaji wa bidhaa zisizoruhusiwa kuingia katika nchi hizo mbili.
Kamishna Mkuu wa URA John Musiujuzi amesema Mamlaka yao na TRA zimekuwa zikipeana mbinu mbalimbali za namna ya kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi ili kuongeza mchango wa Kodi kwenye pato la Taifa.
Amesema URA na TRA zinanufaika na ushirikiano walionao kwa kubadilishana ujuzi, maarifa na rasilimali watu.
Habari Mpya