Emblem TRA Logo

CAG APONGEZA UKUSANYAJI MZURI WA MAPATO MWAKA WA FEDHA 2024/25

31 March, 2026

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25, ambapo jumla ya trilioni 50.29 zilipangwa kukusanywa, huku mapato halisi yaliyopatikana yakifikia trilioni 47.82, sawa na utekelezaji wa asilimia 93.11. Taarifa hiyo inaeleza kuwa mapato ya ndani yaliendelea kuwa mhimili mkuu wa bajeti kwa kufikia asilimia 99.41 ya malengo yaliyowekwa, jambo linaloashiria uimara wa mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato nchini.

Katika mafanikio hayo, Mamlaka ya Mapato Tanzania imetajwa kuwa mchangiaji mkuu, ikionesha utendaji kazi mzuri katika ukusanyaji wa kodi na hata kuvuka malengo iliyopewa. Mafanikio haya yanachangiwa na maboresho ya mifumo ya kidigitali, usimamizi madhubuti pamoja na ushirikiano kati ya walipakodi na mamlaka husika, hali iliyosaidia kuongeza ufanisi na uwazi katika sekta ya mapato.

Aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ameipongeza Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mafanikio hayo, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi hizo ili kudumisha kasi ya ukuaji wa mapato na kuimarisha zaidi uchumi wa taifa.