KAMATI YA BUNGE YA BAJETI YAPONGEZA UTENDAJI KAZI WA TRA
31 May, 2026
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti imeeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuipongeza Mamlaka hiyo kwa utendaji kazi ambao unaiwezesha kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi waliyowekewa na Serikali kwa kila mwezi.
Akizungumza wakati wa kikao baina ya wajumbe wa Kamati hiyo na Menejimenti ya TRA Mei 30, 2026 Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti Mhe. Mashimba Ndaki amesema TRA wanastahili pongezi kwa namna wanavyofanya kazi zao.
Aidha amewapongeza kwa kuwa na Idara maalum ya kuhudumia walipakodi wakubwa hali ambayo itawafanya walipe kodi zaidi na kuijulisha jamii kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika masuala ya kodi na kila anayepaswa kulipa kodi analipa.
"Kumekuwa na dhana kwamba wafanyabiashara wakubwa hawalipi kodi, niwajulishe wananchi kuwa wafanyabiashara wakubwa nao wanalipa kodi ndiyo maana wamewekewa Idara maalumu ya kuwahudumia, na kwenye makusanyo yote ya TRA wanachangia asilimia 40" amesema Ndaki.
Aidha amesema TRA imepiga hatua kubwa kwa kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo ya watumishi wake kuwa na lugha nzuri jambo linalowavutia wananchi wengi kulipa kodi kwa hiari tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo Mamlaka hiyo ilikuwa ikiogopwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Muhandisi Mshamu Ali Munde ameipongeza TRA kwa kuendelea kuongeza wigo wa kodi na kujiweka karibu zaidi na Walipakodi hali ambayo imeongeza uhiari katika kulipa kodi.
Naye Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda ameshukuru hatua ya Kamati ya Bunge kuzitembelea ofisi za Idara ya Walipakodi Wakubwa na kueleza kuwa ziara hiyo itazidi kuwahamasisha Walipakodi hao kuendelea kulipa kodi.
Amesema TRA itaendelea kutenda haki kwa Walipakodi wote kwa kuzingatia madaraja yao kwa yule anayestahili kulipa kikubwa atalipa kikubwa, anayestahili kulipa kidogo atalipa kidogo na yule asiyestahili kulipa hatolipa kwa kuwa huo ndiyo utaratibu wa utendaji wa Mamlaka hiyo.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwafichua wale wanaokwepa kodi ili kila mmoja achangie maendeleo ya nchi.
Habari Mpya