TAASISI ZAIDI YA 300 KUUNGANISHWA NA MFUMO WA IDRAS
21 January, 2026
Kamishna wa Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alfred Mregi amesema Mfumo Mpya Jumuishi wa Kodi za Ndani (IDRAS) utaunganisha mifumo ya taasisi zaidi ya 300 na kurahisisha taratibu zote za ulipaji Kodi.
Akizungumza leo tarehe 21/1/2026 katika semina ya mafunzo ya mfumo huo mpya yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) uliopo Jijini Dar es Salaam Kamishna Mregi amesema, Mfumo wa IDRAS utakua mfumo jumuishi ambao utabeba mifumo mingine zaidi ya 300 ya Taasisi mbalimbali hapa nchini na hivyo kurahisisha taratibu zote za ulipaji wa kodi kwa Walipakodi.
“Taasisi Moja inaweza kuwa na Mfumo wenye Viunganishi (Kiolesura) zaidi ya kimoja, kwa hiyo unaweza kuona kwamba tutaunganisha mifumo mingi sana pengine zaidi ya mia tatu”, amesema Kamishna Mregi
Amebainisha kwamba, mfumo huo unapokwenda kuzinduliwa tayari taasisi zaidi ya 60 zenye mifumo iliyobeba viunganishi viwili na kuendelea imekwisha unganishwa na mara tu baada ya uzinduzi rasmi mifumo itakua tayari kuanza kazi.
Kamishna Mregi amewasisitiza wadau na walipakodi kuhakikisha wanatenga muda wao wa kutosha kuhudhuria mafunzo haya yaliyoandaliwa kwa siku mbili mfululizo, ili kuhakikisha wanapata uelewa stahiki wa kuutumia mfumo huo wa IDRAS.
Ameongeza kuwa, mfumo huo utatumika katika shughuli zote za kodi kama vile usajili, uwasilishaji wa ritani, makadirio ya kodi, ulipaji wa kodi, kazi zote za mapingamizi, rufani za kodi, usimamizi wa madeni, pamoja na usimamizi wa viashiria hatarishi.
“Mfumo huu utajumuisha taratibu zote za unafuu na misamaha ya kodi pamoja na moduli za magari na leseni za udereva,” amesema Kamishna Alfred Mregi.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam Bi. Pendo Lucas ameipongeza TRA kwa kubuni mfumo huu mpya akikiri kuwa, utapunguza kero nyingi za kodi ikiwemo ya makadirio kwa wafanyabiashara. Amewashauri wadau wa kodi na walipakodi kushiriki kikamilifu mafunzo hayo ili wapate uelewa wa kutosha wa kuutumia mfumo huo.
Mfumo wa IDRAS unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 9, 2026 kwa ajili ya kutumika nchi nzima, na utabeba mifumo yote ya makusanyo ya kodi za ndani. Mfumo huo umejengwa kwa zaidi ya miaka miwili mpaka kukamilika kwake.
The Commissioner for Domestic Revenue, Mr. Alfred Mlegi, speaking to participants at a training seminar on the IDRAS system held on 21/1/2026 at the Mwalimu Nyerere Hall located at Posta, Dar es Salaam City.
Habari Mpya