IMF YAIPONGEZA TRA KWA UFANISI MZURI KATIKA USIMAMIZI WA KODI
04 May, 2026
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utendaji na ufanisi mzuri katika usimamizi wa ukusanyaji wa kodi nchini ambao umeongeza uhiari katika kulipa kodi sambamba na ongezeko la makusanyo ya kodi katika mwaka wa fedha 2025/26.
Pongezi hizo zimetolewa na ujumbe wa IMF, ukiongozwa na Bw. Nicolas Blancher, walipofanya mazungumzo na uongozi wa TRA chini ya Naibu Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Mcha Hassan Mcha Mei 04, 2026 katika ofisi za Mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo ujumbe wa IMF ukiongozwa na Bw. Blancher wamesema TRA imekuwa ikifanya kazi nzuri na kwa ufanisi mkubwa hali ambayo imesababisha utulivu katika ukusanyaji wa kodi na kuondoa malalamiko kwa walipakodi jambo ambalo ni la kupongezwa.
Katika mazungumzo hayo ujumbe wa IMF umesema upo tayari kushirikiana na TRA katika kuwajengea uwezo watumishi wake kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo usimamizi wa kodi kwenye sekta ya uzalishaji na viwanda na katika kuangalia namna bora ya kurasimisha sekta isiyo rasmi.
IMF pia itaiwezesha TRA kutoa mafunzo ya uendeshaji wa maabara za Forodha pamoja na utekelezaji wa mpango mkakati wa kuongeza uhiari wa kulipa kodi.
Kwa upande wa TRA, Naibu Kamishna Mkuu Bw. Mcha Hassan Mcha ameishukuru IMF na kueleza kuwa ushirikiano huo utakuwa na tija kwa TRA kwa kuwaongezea ujuzi watumishi wake ili waendelee kutoa huduma bora kwa walipakodi.
Naibu Kamishna Mkuu Mcha amesema eneo la kuwajengea uwezo watumishi wa TRA litakuwa na tija kubwa na kuwa IMF imekuwa na uhusiano mzuri na TRA kwa muda mrefu sasa jambo ambalo limeonyesha tija katika utekelezaji wa majukumu yao.
Habari Mpya