Emblem TRA Logo

KAMISHNA MKUU MWENDA AAHIDI TRA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WALIPAKODI

23 May, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo itaendelea kutoa huduma bora kwa Walipakodi nchini ili kuhamasisha ulipaji kodi kwa hiari.

 Ameyasema hayo Mei 23, 2026 akiwa ziarani katika wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kueleza kuwa TRA ipo kwaajili ya wananchi hivyo kutoa huduma bora ni wajibu wao. Amesema lengo la TRA ni kukuza ulipaji wa kodi kwa hiari kwa kuwafanya wananchi waone fahari kulipa kodi na kuongeza wigo wa kodi kwa kusajili walipakodi wapya sambamba na kurasimisha biashara ambazo bado hazijarasimishwa.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaendelea kuwezesha biashara nchini kupitia Dawati maalumu la uwezeshaji Biashara, kuwasikiliza walipakodi na kutatua changamoto zinazowakabili huku akitoa wito kwa Mameneja wa TRA kwa mikoa yote kutoka ofisini na kuwafuata walipakodi kwenye maeneo yao na kuwasikiliza. 

"Ni wajibu wetu kutoa huduma bira kwa walipakodi na kuwezesha biashara zao maana bila wao sisi hatuwezi kuwepo" amesema Bw. Mwenda. Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya Bw. Musibu Shabani amesema mkoani humo wameendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na walipakodi hali ambayo imewawezesha kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi kwa mwaka miezi 10 mfululizo ya mwaka wa fedha 2025/2026. Bw. Musibu ameahidi kuendelea kuboresha zaidi utoaji wa huduma za kodi na kukuza ulipaji wa kodi kwa hiari mkoani humo kwa kushirikiana na walipakodi huku wakiwatembelea kuwasikiliza na kutatua changamoto zao kwa wakati