BANDARI KAVU SASA KUFANYA KAZI SAA 24
23 February, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yusuph Juma Mwenda amewataka wamiliki na waendeshaji wote wa Bandari Kavu nchini (ICD) kuanza kufanya kazi saa 24 ili kuendana na kasi ya utoaji wa huduma za Forodha.
Akizungumza Februari 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha pamoja na wamiliki wa ICDs Kamishna Mkuu Mwenda amesema kufanyika kwa kazi saa 24 kutarahisisha Zaidi biashara na kuondoa msongamano wa mizigo na kuwa wapo tayari kuwezesha kuanza kwa utaratibu huo ambao kwa upande wa watumishi wa Forodha tayari umeanza.
Amesema anatambua umuhimu wa ICDs na mchango wao katika makusanyo ya kodi maana wamekuwa wakiwezesha na kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi.
"Niwatake kuhakikisha mnaongeza ufanisi katika ufanyaji wenu wa kazi kwa kujipanga kutoa huduma kwa Saa 24, sisi kama TRA tutatoa wafanyakazi wetu nanyi kwa upande wenu mjipange kwa vifaa na mengineyo, lengo ni kuongeza ufanisi" Amesema Mwenda.
Amesema ufanisi wa bandari kavu unakwenda sambamba na ufanisi wa Forodha hivyo ni wajibu wa wamiliki kushirikiana na TRA kuongeza ufanisi wa pamoja huku akiwapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda ameonya vitendo vya ukwepaji kodi vinavyofanywa na baadhi ya Wamiliki wa Bandari hizo akisisitiza kuwa TRA inazo taarifa za vitendo hivyo na kwamba haitosita kuwachukulia hatua.
"Natambua kuna ukwepaji kodi katika ICD, hii haiwezi kukubalika, ICD zote zinatakiwa kuzingatia Sheria, ni lazima tushirikiane kuzifanya ICD zionekane kuwa ni salama, hatutosita kuchukua hatua kwa wale watakaobainika" amesisitiza Mwenda
Awali akizungumza katika kikao hicho Rais wa Sekta Binafsi (TPSF) Bi. Angelina Ngalula amesema waendeshaji bandari kavu ni kiungo muhimu katika uchumi kuelekea Dira ya Taifa ya 2050 wanapaswa kuungana na kushiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi kwa kuleta mapinduzi chanya.
Habari Mpya