Emblem TRA Logo

KAMISHNA MKUU MWENDA AKUTANA NA WAAGIZA MAFUTA ZANZIBAR, ATOA UTARATIBU MPYA

18 March, 2026

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda amekutana na wafanyabiashara wanaoagiza mafuta ya kupikia nje ya nchi kupitia Visiwani Zanzibar na kuyasafirisha kwenda Tanzania Bara na kuwapa utaratibu mpya wa kuingiza mafuta hayo.

Akizungumza na wafanyabiashara hao katika kkkao kilichofanyika Machi 17.2026 Visiwani Zanzibar Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA itaanza kutekeleza utaratibu mpya wa utolewaji wa vibali vya kuingiza mafuta Tanzania Bara kutoka Zanzibar. 

Amesema utaratibu huo utatoa punguzo la kodi kwa wafanyabiashara hao ili kuwawezesha kupata faida lakini kutakuwa na kiwango maalum cha kuingiza ili kulinda viwanda vya ndani na vibali vitatolewa kwa upungufu uliopo pekee.

Amesema kuanza kwa utaratibu huo kutaongeza ufanyaji kazi wa Bandari za Bagamoyo, Mbweni na Kunduchi na kuwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa kutakuwa na uwazi katika utoaji wa vibali hivyo vya uingizaji wa mafuta ya kupikia kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara.

"Niliunda Timu kwaajili ya kutafuta suluhisho la uingizaji wa mafuta ya magendo ambayo ilishirikisha wazalishaji wa ndani, waingizaji wa mafuta na wataalam kutoka TRA ambayo imekuja na mapendekezo yanayolenga kuondoa tatizo la uingizaji wa mafuta ya magendo" amesema Bw. Mwenda. 

Amesema lengo la kuweka udhibiti huo ni kutaka kulinda viwanda vya ndani, kuwezesha biashara, kulinda afya za wananchi na kukusanya kodi ili kuwezesha Serikali ipate sehemu yake na Walipakodi nao wapate sehemu yao.

Akizungumza katika kikao hicho Mfanyabiashara wa mafuta ambaye huagiza kutoka nje ya nchi Hassan Said Ngozi amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA na kuipongeza Mamlaka hiyo kwa kuja na uamuzi huo utakaowezesha kuendelea kwa biashara zao maana walisimama kusafirisha ili kusubiri muongozo.