KAMISHNA MKUU ATOA RAI KWA WAHARIRI KUFICHUA WANAOKWEPA KODI, AWASHUKURU KWA USHIRIKIANO WA MIAKA 30
29 June, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda ametoa rai kwa Wahariri na Waandishi wa Habari nchini kushiriki katika kuwafichua wakwepa kodi ili kuisaidia nchi huku akiwashukuru kwa kushirikiana na TRA kwa kipindi chote cha miaka 30 cha uhai wake.
Ametoa ombi hilo na pongezi wakati wa Mkutano baina yake na Wahariri uliofanyika jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya TRA na utoaji wa Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora zinazotarajiwa kutolewa Julai Mosi mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema vitendo vya ukwepaji wa kodi vimekuwa vikidhoofisha uchumi wa nchi na kuondoa ushindani sokoni hivyo Wahariri wakishiriki kuwafichua wakwepa kodi watakuwa wameisaidia nchi.
Amesema katika kipindi cha miaka 30 ya uwepo wa TRA njia za kidijitali za ukwepaji kodi zimekuwa zikitafutwa na kupitia mfumo mpya wa usimamizi wa kodi za ndani IDRAS TRA itaweza kufuatilia walipakoadi wote kwa kushirikiana na Taasisi nyingine ambazo mifumo yake inasomana na mifumo ya TRA.
Amesema kwa miaka 30 TRA imefanikiwa kuwa karibu zaidi na Walipakodi hali ambayo imeongeza ulipaji kodi kwa hiari na imani ya walipakodi kwa TRA na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa kwa makusanyo ya kodi zinazokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.
Kamishna Mkuu Mwenda ametumia mkutano huo kuwashukuru Walipakodi kote nchini kwa kuendelea kulipa kodi sambamba na Wahariri na kueleza kuwa mafanikio ya TRA yanayozungumzwa hayawezi kuwepo bila walipakodi Wazalendo.
Habari Mpya