TUENDELEE KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIKANDA KATIKA USIMAMIZI WA MAPATO NA KUZUIA MAGENDO - CG MWENDA
24 September, 2026
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda miongoni mwa mamlaka za mapato za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto za usimamizi wa kodi, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwezesha biashara katika ukanda huo.
Kamishna Mkuu Mwenda, ameyasema hayo leo wakati akishiriki Kikao cha 54 cha Makamishna Wakuu wa Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki (EARACGS) kilichofanyika kwa njia ya mtandao, ambapo amesisitiza umuhimu wa kubadilishana taarifa, uzoefu na mbinu bora, pamoja na kuimarisha mifumo ya ndani ya usimamizi wa kodi na kupambana kwa pamoja na biashara za magendo.
Aidha, amesisitiza kuboresha huduma za forodha na kuharakisha uondoshaji wa shehena katika vituo vya mipakani ili kurahisisha biashara zinazovuka mipaka, huku akieleza umuhimu wa nchi wanachama kushirikiana katika kutatua changamoto zinazohusu utekelezaji wa mfumo wa pamoja wa viwango vya ushuru na kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika kila nchi.
Kikao hicho cha 54 cha EARACGS kimejadili ufanisi wa mamlaka za mapato katika mwaka wa fedha 2025/26, utozaji wa kodi katika sekta isiyo rasmi, njia mbadala za kushughulikia mapingamizi ya kodi nje ya mahakama, pamoja na ukusanyaji wa kodi katika uchumi wa kidijitali na mali za kidijitali (digital assets).